Serikali imetoa Shilingi bilioni 286 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu Mkoani Arusha uliopewa jina la Dokta Samia Suluhu Hassan utakaojengwa na Kampuni ya CRCEG kutoka nchini China.
Ameyanena hayo leo Machi 19, 2024 Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa uwanja huo, na kusema kuwa, uwanja huo utaingiza watu 30,000 na kudai utakuwa uwanja wa kisasa zaidi katika Afrika Masharika.
Alisema Serikali itahakikisha ujenzi huo unafanywa kwa haraka kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ifikapo mwaka 2027, ikiwa ni juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Alisema uwanja huo utachagiza kwa kiasi kikubwa utalii wa nchi yetu kwani zitafanyika shughuli mbalimbali tofauti na mpira wa miguu kama vile mchezo wa riadha, pamoja na biashara zitakazokuwa zinafanyika uwanjani hapo.
“Uwanja huo utakuwa na ubora wa hali ya juu kwani utakuwa na vyumba vya watu mashuhuri pande zote mbili za uwanja zoezi hili limefanyika leo ambapo, Rais Samia akiwa anatimiza miaka mitatu ya uongozi wake, alisema Ndumbaro.
Aidha aliipongeza Kamati ya kudumu ya Bunge ya elimu Utamaduni na Michezo kwa juhudi iliyofanya mpaka kukamilisha zoezi hilo ambalo limechukua muda mrefu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Husna Sekiboko amewataka wakandarasi wa uwanja huo wahakikishe ujenzi unakamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Wakandarasi hakikisheni kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025 uwanja uwe umefikia kiwango kinachoridhisha na utekelezaji huo uanze haraka iwezekanavyo ikiwa ni maandalizi kuelekea katika michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON),”alisema.
Amesema Kamati itatoa ushirikiano kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kama ilivyokusudiwa na kudai kuwa, Rais Samia anaitendea haki sekta ya michezo kama anavyofanya kwenye sekta nyingine, na kuwataka watu wa Arusha watunze rasilimali za uwanja huo.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela alisema uwanja huo utaongeza idadi ya watalii katika Mkoa huo.