Kocha mkuu wa kikosi cha Mamelodi Sundowns Rhulan Mokwena ameweka wazi kuwa timu yake itafuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Barani Afrika licha ya kutoa sare [0-0] na Yanga kwenye mchezo wa kwanza wakiwa ugenini.
“Yeah nafikiri mtaiona Mamelodi Sundowns kwenye hatua inayofuata” – Mokwena.
“Nina uhakika na hilo, kiukweli, mipango ni nini ?, mipango ni kufika nyumbani salama kwasasa, tumpumzike, tunywe maji mengi, tulale, tuutazame tena mchezo na tujiandae na Richards Bay” – Mokwena
“Tuna mchezo muhimu sana wa LigiJumanne hii, huo ndio mpango wangu kwasasa” – Mokwena.
Mamelodi Sundowns jana imecheza mchezo wake wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Yanga bila ya nahodha wake Themba Zwane ambaye alikuwa na kadi za njano alizozipata kwenye hatua ya makundi.
Mokwena ameeleza kuwa kukosekana kwake kumemfanya ashindwe kutekeleza vyema mbinu zake na anatarajia kuwa naye kwenye mchezo wa marejeano utakaofanyika Pretoria Afrika Kusini.
“Ni nahodha wa timu, ni mtu mhimu sana kwenye timu yetu” – Mokwena.
“Bila shaka tumekosa huduma yake kiasi leo lakini kila mmoja amefanya kwa nafasi yake, nimefurahishwa na majitoleo na upambanaji wa timu, hasa hasa kipindi cha pili” – Mokwena.
“Sio rahisi kutoka kwenye michezo ya FIFA lakini tumejaribu, huu ni mchezo wa kwanza baada ya mapumziko ya kimataifa, lakini ni sawa acha tuone itakavyokuwa” – Mokwena.
Mchezo wa Yanga na Mamelodi Sundowns umeshika vichwa vya habari na kuzungumzwa zaidi nchini Tanzania na Afrika Kusini ukiwakutanisha mabingwa wawili wa Ligi mbili kubwa.