Ikiwa ni saa mbili kamili usiku kwa saa za Afrika Kusini ni saa tatu usiku kwa saa za Tanzania, wajukuu wa Nyerere watakuwa kwenye kibarua kizito cha kuipeperusha bendera ya nchini wakiwa ugenini.
Ni mara ya pili Yanga inaenda nchini Afrika Kusini kucheza mchezo wa mtoano kwenye michuano ya Afrika, mara ya kwanza wakienda kucheza msimu uliopita nusu fainali ya pili dhidi ya Marumo Gallants na wakaondoka na ushindi.
Mara hii wanaingia kucheza dhidi ya Mamelodi Sundowns kwenye dimba la Loftus Versfied lililopo Pretoria nchini Afrika Kusini, huu ni mchezo mhimu zaidi kwa klabu ya Yanga kwani matokeo wanayohitaji ni ushindi au sare yenye magoli ili wafuzu hatua inayofuata.
Mchezo wa Yanga na Mamelodi unatazamwa zaidi kutokana na ubora wa hivi karibuni wa timu zote mbili, Yanga ikifika fainali ya kombe la Shirikisho msimu uliopita huku Mamelodi wakitwaa ubingwa wa AFL msimu huu.
Kuelekea mchezo huo mhimu klabu ya Yanga inatarajiwa kuendelea kuwakosa nyota wake muhimu waliokosekana pia kwenye mchezo wa awali uliochezwa Dar Es Salaam.
Kocha mkuu wa Yanga Miguel Gamondi ameeleza kuwa leo kutakuwa na urejeo wa nyota mmoja kwenye kikosi huku inatajwa mlinzi wa kulia Yao Attohoula hatakuwa sehemu ya kikosi huku Aucho akipewa nafasi ndogo ya kuwepo kwake lakini Pacome Zouzoua anatajwa kurejea kwenye kikosi hii leo.
“Kwenye Wachezaji wangu watatu ambao ni majeruhi kuna uwezekano mkubwa wa mmoja kati yao kucheza kesho, ila wengine sipo tayari kuharakisha kuwatumia kwakuwa Yanga haichezi klabu bingwa pekee bali tuna michuano mingine, afya yao ni kitu muhimu zaidi kwangu kuliko kuwahisha kuwatumia hapo kesho, ni suala la afya nami ni Binadamu napaswa kuthamini hilo”
- Coach Miguel Gamondi wa Yanga kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Sundowns.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizi mbili kukutana kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya mabingwa Barani Afrika na pengine mchezo wa leo utafuatiliwa zaidi na wapenzi wa soka kwani ndio mchezo wa maamuzi kwa pando zote mbili huku Mamelodi Sundowns ikiwa na faida ya kucheza ugenini.