Connect with us

NBC Premier League

SIMBA WAKWAMA LITI, JKT TANZANIA WAKIWATIBULIA TABORA UNITED

Klabu ya Soka ya Simba imeshindwa kuibuka na alama 3 mbele ya Ihefu kwenye mchezo uliokuwa na ushindani wa aina yake uliomalizika kwa sare ya 1-1 mchezo uliopigwa kwenye dimba la CCM Liti na kujikuta wanasalia nafasi ya 3 wakifikisha alama 46, 1 nyuma ya Azam walio nafasi ya 2.

Licha ya Simba kuuanza mchezo kwa nguvu wakitengeneza nafasi nyingi za mapema lakini bado washambuliaji wake hawakuwa makini kwenye kuzitumia nafasi zao huku pia walinzi wa Ihefu wakiwa makini kuzuia hatari hizo.

Freddy Kouablan alipata nafasi ya mapema zaidi lakini alichelewa kufanya maamuzi akiwa anamtizama tu Aboubakar Khomeiny lakini Benjamin Tanimu akawahi na kufanya uokovu.

Saido Ntibazonkiza pia alitengenezewa nafasi nzuri na Clatous Chama lakini shuti lake halikuwa na nguvu na kuishia mikononi mwa golikipa Aboubakar Khomeiny.

Simba waliadhibiwa kwa kushindwa kuchukua nafasi zao dakika ya 41 ya mchezo baada ya Ihefu kupata bao la utangulizi kupitia kwa Duke Abuya akipokea pasi nzuri kutoka kwa Elvis Rupia wakiwakamata Simba kwenye mpira wa kushtukiza wakiwa na namba chache kwenye eneo lao la Ulinzi na akiwa kwenye utulivu wa hali ya juu akaweka kambani.

Mpaka mapumziko Simba walikuwa nyuma kwa bao 1-0.

Dakika 45 za kipindi cha pili ziliendelea kutawaliwa na Simba lakini changamoto ikaendelea kuwa kushindwa kutumia nafasi.

Simba walipata bao la kusawazisha dakika ya 72 kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya Kibu Denis kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la 18 na penati kufungwa na Clatous Chama.

Dakika 90 zikatamatika kwa Simba na Ihefu wote kuondoka na alama 1.

Kocha Selemani Matola alisema kuwa :

Nadhani tumecheza vizuri lakini hatukuweza kutumia nafasi tulizozitengeneza pengine tungezitumia tungeibuka na ushindi na nadhani tulistahili kushinda. Sisi tumefanya makosa wametuadhibu ndio mpira. Lakini bado tupo kwenye mbio za Ubingwa na ili tuone mwanga lazima tushinde mchezo ujao wa Derby

Naye Kocha Mecky Mexime alisema haya :

Unajua unapocheza na Simba lazika uwe makini sana na ucheze kwa mbinu mno. Watu wanaweza wakawaona Simba kama wabovu hii ni hali tu wanapitia lakini kwenye uwanja ni timu Bora sana. Sisi tuliona hatuwezi kupishana nao ndio maana tukaamua kuwaacha wacheze lakini tuzuie kwenye eneo letu bahati nzuri hawakuwa na wachezaji wenye ubunifu hasa walipomtoa Chama na sisi tukapumua. Binafsi mimi naona nimefanikiwa zaidi

Simba wamefikisha mechi 4 bila ushindi wowote kwenye mashindano yote.

Kwingineko kwenye Dimba la Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Bao la dakika za mwisho kabisa lilifanya mchezo kati ya wenyeji Tabora United na JKT Tanzania kumalizika kwa sare ya 1-1.

Tabora United walitangulia kupata bao dakika ya 72 kupitia kwa Lulihoshi kabla ya JKT Tanzania kusawazisha dakika za mwisho kabisa.

JKT Tanzania wanapanda mpaka nafasi ya 12 wakifikisha alama 21 wakiwazidi timu 3 zenye alama 21 pia, Mashujaa, Tabora United na Geita Gold kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League