Bodi ya Ligi kuu kandanda Tanzania Bara imefanya maboresho kwenye ratiba ya michezo mbalimbali ya Ligi kuu. TaarIfa kutoka bodI ya ligi imeeleza sababu za maboresho hayo ni kuongeza ufanisi katika michezo ya Ligi na ushiriki wa klabu kwa ujumla ambapo masuala kadhaa yamezingatiwa yakiwemo kuondolewa kwa klabu za Azam na Singida katika michuano ya kimataifa, ushiriki wa Simba na Yanga kwenye michuano ya Kimataifa.
Sababu nyingine ni kutokuwepo kwa michezo ya kuwania kufuzu fainali za AfriKa kwa wachezaji wa ndani (CHAN), ambayo hadi sasa ratiba yake haijatangazwa na tayari kipindi kilichotengwa kwa michezo ya awali kimepita bila michezo hiyo kuchezwa .
Baada ya maboresho hayo mchezo wa Young Africans dhidi ya Azam uliopangwa kuchezwa October 25 sasa utapigwa October 22 katika dimba za Azam Complex saa 12:30 Jioni, ikiwa Yanga ndio mwenyeji wa mchezo huo.
Mchezo mwingine wa Young Africans ni dhidi ya Singida uliokuwa umepangwa kupigwa October 29 sasa utapigwa October 26 uwanja wa Azam Complex saa 12:30 Jioni, huku mchezo wa Simba dhidi ya Young Africans utasalia tarehe ileile ya awali November 5.
Klabu ya Simba itakuwa na michezo miwili pekee ambayo tarehe yake inajulikana kwenye ratiba kuanzia sasa hadi mwezi wa kwanza, itacheza dhidi ya Young Africans November 5, saa 11 Jioni katika uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya hapo watakutana na Tabora United, December 29 saa 10 Jioni katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora. Ratiba ya michezo mingine ipo hapo chini.