MTIBWA SUGAR : 4-2-3-1: Mchezo wa 6 bila Kuvuna alama 3 huku wakishindwa kabisa kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kwa kuvuna alama 1 tu pekee(Dhidi Coastal Union) huku wakifungwa mchezo wa 3 leo(Pia dhidi ya Simba na Singida FG). Ila zaidi kinachotia hofu ni uchezaji wa timu, bado haionekani wakicheza kimalengo.
Safu ya ulinzi ilifanya makosa mengi sana hasa kipindi cha kwanza, licha ya kucheza vizuri dakika za mwanzo hapakuonekana mawasiliano mazuri kati ya Luseke Kiggi na Oscar Masai licha ya kucheza pamoja muda mwingi, walisababisha kijana Nickson Joseph kuwa na wakati mgumu na upande wake kutumika sana kuanzishia mashambulizi, alitamba sana Gasper Mwaipasi eneo hili. Lakini hata upande wa Yusuf Mustapha palikuwa panapitika kirahisi. Haikuwa rahisi kuamini kuwa Ally Nassor “Ufudu” ambaye sio winga kiuhalisia kuonekana aking’ara mbele ya beki mzoefu na dakika ya 31, akawaadhibu kutokana na makosa hayo.
Walijaribu kurejea kipindi cha pili lakini Kagera walikitawala zaidi na kulazimishwa kufanya makosa zaidi. Nafasi kadhaa walijaribu kutengeneza lakini walishindwa kuzitumia Mtibwa Sugar, sio Matheo Anthony, Seif Karihe, Kelvin Nashon wala Ladack Chasambi walioonyesha cheche zao leo mbele ya ngome imara ya Kagera. Hata Mwalimu Awadh alipojaribu kuwaingiza Abalkassim, Marungu na Juma Luizio kwenye safu ya Ushambuliaji, bado hali ilikuwa tete mpaka dakika 90 zinamalizika.
KAGERA SUGAR : 4-4-2: Mecky alijua awashike wapi Mtibwa Sugar, alijaza viungo wengi. Cleophace Mkandala, Gasper Mwaipasi, Abdallah Seseme, Nicholaus Kasozi, Ally Nassor Ufudu wote ni viungo asilia na wenye uwezo wakucheza kukaba na kushambulia huku mshambuliaji asilia akiwa ni Obrey Chirwa tu kwenye safu ya ushambuliaji.
Hii iliwanyima uhuru walinzi wa pembeni hasa wa Mtibwa kupandisha mashambulizi na kurahaisisha kazi kwa Kagera. Anapokuwepo mtu kama Ufudu kwenye kiungo halafu anacheza kama winga inakupa vitu viwili kutoka kwake, ulinzi na ushambulizi. Datius Peter alikuwa likizo hasa kipindi cha pili. Ilikuwa sawa upande wa Mwaipasi, alimmpa wakati mgumu sana Nickson Joseph na hasa ukizingatia hakuwa akiupata usaidizi wa kutosha kutoka kwa Ladack Chasambi.
Kuongezeka kwa vijana Said Naushad, Hijjah Shamte, Abiud Mtambuku na Said Omary Natepe kipindi hiki cha pili kuongeza nguvu kwa Chirwa ni kama palichochea zaidi moto, na kuipoteza zaidi Mtibwa. Dakika ya 90 kijana Natepe ambaye aliingia dakika chache zilizopita akaifungia Kagera goli la pili na kupigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Mtibwa Sugar.
MAANA YAKE
Mtibwa anazidi kudidimia zaidi kwenye msimamo wa ligi kuu akiwa nafasi ya mwisho ya 16 akibaki na alama zake 2 huku Kagera Sugar akisogea hadi nafasi ya 6 akiwa na alama 8. Hali sio nzuri kwa Mtibwa Sugar.
NYOTA WA MCHEZO:
ALAINE KATENGUA(KAGERA SUGAR); Alikuwa mtulivu sana golini dakika zote na pia aliweza kuchezesha timu yake. Akiwapanga vizuri mabeki wake wasifanye makosa yasiyo ya lazima lakini pia aliweza kushinda mipira mingi ya kugombania hewani.