Ligi

GEITA GOLD, DODOMA JIJI HAKUNA MBABE NYANKUMBU

Published on

Geita Gold walikosa nafasi ya Kupanda hadi nafasi ya 9 kwenye msimamo wa NBC Premier League baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Dodoma Jiji kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Nyankumbu.

Walikuwa ni wenyeji Geita Gold waliotangulia kupata bao dakika ya 10 tu ya mchezo kupitia kwa Tariq Seif Kiakala aliyeusokomeza kimiani mpira kwa kichwa kufuatia mpira uliokuwa ukizingeazengea kwenye lango la Dodoma Jiji, baada ya krosi nzuri kutoka kwa  Offen Chikola kushindwa kuokolewa vizuri.

Dodoma Jiji walicharuka kutaka kusawazisha lakini ngome ya ulinzi ya Geita Gold ilikuwa imara kuzuia mashambulizi. Mpaka wanakwenda mapumziko Geita wakawa mbele kwa 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Mwalimu Melis Medo alimuingiza Hassan Mwaterema kwenda kuongeza nguvu ya mashambulizi na ilizaa matunda kwani dakika ya 62, Alimalizia mpira uliokuwa ukielekea langoni kutoka kwa Emmanuel Martin baada ya uzembe wa mabeki na golikipa Erick Johora kushindwa kudhibiti krosi iliyochongwa na Gustapha Saimon Lunkombi.

Hassan Mwaterema aliwainua tena wageni  dakika ya 65 baada ya kufanya muunganiko mzuri tena na Emmanuel Martin baada ya kazi nyingine nzuri kutoka kwa Gustapha Saimon aliyepiga pasi ndefu pembeni kwa Emmanuel Martin na kupiga krosi ya chini iliyomaliziwa kiustadi na Hassan Mwaterema. Mbadiliko yakalipa.

Wakati watu wote uwanjani wakidhani mechi imelala hivyo , Hassan Mahmoud alikuwa na mawazo mengine tofauti. Dakika ya 86 ya mchezo, aliwasawazishia Wachimba Dhahabu na kuwapa alama muhimu kwenye mchezo huu ulioonekana kuwatoka.

Mchezo mzuri ulikuwa wenye shehena ya magoli na ufundi mwingi pia hasa kwenye eneo la kiungo. Mpaka filimbi ya mwisho ya mchezo, Geita Gold 2-2 Dododma Jiji.

Popular Posts

Exit mobile version