Mchezaji wa mpira wa Kikapu, Hasheem Thabeet anatarajiwa kuiongoza timu yake ya Pazi anayoichezea kwa muda kwenye mchezo wao wa 3 leo jioni hii dhidi ya timu ya Mamlaka ya Bandari ya Kenya( KENYA PORTS AUTHORITY BBC) ikiwa ni mfululizo wa michezo ya kushindania nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mpira wa kikapu Afrika, BAL(BASKETBALL AFRICA LEAGUE)
Pazi ni wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano haya ya mchujo yanayofanyika kwenye viwanja vya IST Gymnasium, Dar es Salaam, Tanzania ili kupata timu 12 zitakazokwenda kuchuana kwenye michuano ya BAL 2024 ambayo ipo chini ya FIBA pia.
Tayari Hashim ameiongoza timu yake ya Pazi kushinda michezo miwili, na mchezo wa jana dhidi ya DYNAMOS ya Burundi waliwafunga kwa vikapu 71-62 mchezo ulioshuhudia nyota wa Ufaransa aliyeichezea timu ya Le Mans mwaka 2019 kwenye michuano ya ligi ya mabingwa ulaya ya mpira wa kikapu, Louis Rucklin wa Pazi akiwa MVP wa mchezo huo.
Hashim alisema kuwa yuko nchini kwa ajili ya mapumziko huku akisikilizia simu ziite na kuichezea Pazi kwenye michuano sio tu kwa ajili ya mazoezi ya kujitengenezea njia ya kutafuta timu bali ni Uzalendo.