Mpira ulianza taratibu dakika 15 za mwanzo kila timu ikimmsoma mpinzani wake. Sio prisons wala JKT waliopeleka mashambulizi ya nguvu kwa mpinzani wake. Ikiatarajiwa kuwa mchezo wenye nguvu na rapsha za hapa na pale, mchezo wenyewe ulikuwa na utulivu mkubwa huku mikakati kipangwa taratibu.
Salum Mashaka Kimenya alipiga mpira kama krosi kutokea eneo la kulia la Prison dakika ya 17, huku mipra ukionekana kama haujalenga madhara, lakini ilimlazimu golikipa Ismail Samwel kufanya kazi ya ziada kuokoa hatari langoni mwake.
Dakika ya 19, Edwin Balua alitaka kukumbukia alichokifanya dhidi ya Simba kwa kupiga mpira uliokufa langoni mwa JKT lakini mpira ukagusa nyavu za nje. Kwa takribani dakika 5, Prisons walilisakama sana goli la wapinzani wao.
JKT walijaribu kujibu mashambulizi, na dakika ya 24, Edward Songo alipokea pasi tamu kutoka kwa Najim Magulu lakini shuti lake hafifu liliokolewa kiuepesi na golikipa Yona Amos.Wakati huu JKT waliwafanyia shinikizo kubwa Prisons.
Mpira uliongeza kasi dakika hizi za kipindi hiki cha kwanza JKT wakishambulia, Prisons wanajibu ikizidi kuonekana njaa ya kutafuta bao kwa timu zote mbili. Kuotea mara 8 na Mashuti 6 kwa ujumla wao mpaka dakika ya 40 ya mchezo ilithibitisha hili, kasoro tu goli kupatikana.
Wakati ikionekana kama kuna uwezekano wa kwenda mapumziko 0-0, JKT Tanzania wakiwa wana umiliki wa mpira kwa asilimia 52 dhidi ya 48 za Prison, walipata goli la Kuongoza kupita bao la kujifunga la Salum Kimenya dakika ya 41. Kazi nzuri kwenye eneo la kiungo kutoka kwa Said Ndemla akapiga pasi pembeni kushoto kwake kwa Sixtus Sabilo aliyemmtengea pasi nzuri David Brayson na kupiga shuti dogo la chinichini, lililombabatiza mlinzi wa Prisons, Salum Kimenya na kummpotezea uelekeo Yona Amos na mpira kujaa kimiani. Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinatamatika, 1-0 JKT Tanzania.
Kipindi cha pili kilianza kwa Prisons kufanya mabadiliko ya kiufundi kwa kummtoa Messi Roland Atangana ambaye alionekana kutokwenda sawa na kasi ya mchezo siku ya leo na kuingia Zabona Mayombya na haikummchukua muda kwani dakika ya 47 tu ya mchezo aliachia shuti kali lililotoka pembeni kidogo mwa langa la JKT Tanzania. Kitu walichokikosa Prisons kipindi cha kwanza.
Kuingia kwa Zabona kuliongeza kasi ya mashambulizi kwa Tanzania Prisons, wakiwa washambuliaji wanne, pamoja na Jeremiah Juma Mgunda, Edwin Charles Balua na Beno Khalfan Ngassa, mdogo wa Mrisho Khalfan Ngassa ambaye alitoka na kummpisha Mambote Batshie dakika ya 61 ambaye ana asili ya ushambuliaji kama alivyo Beno. Prisons walikuwa wanasaka kweli goli la kusawazisha dakika hizi. Huku JKT Tanzania nao wakimmpumzisha Edward Songo na Kumuingiza Mohamed Bakari.
Almanusura Prisons wapate goli la kusawazisha dakika ya 64 baada ya Jeremiah Juma kushindwa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Edwin Balua aliyeachia shuti kali la chinichini kama krosi dongo na ilihitaji mguso tu wa Mfungaji lakini akaukosa kabisa na kuushuhudia mpira ukienda nje. Nafasi ya dhahabu hii walikosa Prisons.
Dakika ya 69, Jeremiah Juma alisahihisha makosa yake kwa kuisawazishia timu yake baada ya kuunganisha kiustadi kwa kichwa krosi maridadi ya Zabona Mayombya. Goli lake la kwanza la msimu huu kwa Jeremiah. Prisons walionyesha kuitaka mechi mpaka muda huu. Waliuchukua zaidi mchezo huu kipindi cha pili.
Sare ya 3 kati yao kwenye michezo 8 waliyowahi kukutana ilionekana kunukia mpaka dakika ya 83 ya mchezo. JKT wakafanya mabadiliko kwa kumuingiza Hassan Dilunga nafasi ya Najimu Magulu kujaribu kusukuma mashambulizi mbele lakini bado haikuzaa matunda. Kila timu ilijitahidi kuwa imara dakika za mwisho, kulinda kwanza kilichopo na kutafuta kingine taratibu.
Mpaka kipyenga cha mwisho cha Muamuzi Heri Sasii kinapulizwa, TANZANIA PRISONS 1-1 JKT TANZANIA. Kwa matokeo haya Prisons wanasalia nafasi ya 13 lakini JKT Tanzania watasogea hadi nafasi ya 9 kutoka nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi kuu ya NBC.