Ripoti zinaeleza kuwa nyota wa timu ya Taifa ya Germany na klabu ya Bayern Munich Jamal Musiala anaweza kufikiria uwezekano wa kuhamia Real Madrid ama Manchester City iwapo ndoto zake za kubeba ubingwa wa Ligi ya mabingwa Barani Ulaya (UEFA) na Tuzo za mwanasoka bora Duniani za Ballon d’Or hazitatimia akiwa na klabu ya Bayern Munich.
Kwa upande wa Musiala, 20, anasema hana mpango wa kuondoka Bayern katika kipindi cha hivi karibuni lakini anaweza kufukiria kuondoka ifikapo mwaka 2025, kama hataweza kufikia malengo yake akiwa na Bayern Munich.
Mkataba wa Jamali Musiala na klabu ya Bayern Munich utakaomalizika mwaka 2026, una thamani ya €9m kwa mwaka, kiwango ambacho kinaweza kufikiwa na klabu kama Real Madrid na maongezi kuhusiana na mkataba mpya hayatafanyika hivi karibuni.
Rais wa klabu ya Real Madrid Florentino Perez anahitaji Musiala acheze sambamba na rafiki yake wa karibu Jude Bellingham, nyota ambaye alisajiliwa kutoka Ligi ya Bundesliga msimu uliopita wa kiangazi.
Musiala alianza maisha yake ya soka katika klabu ya vijana ya Southampton na Chelsea kabla ya kuijiunga na Bayern akiwa na umri wa miaka 16.