Klabu ya Inter Miami imethibitisha kuachana na nyota wake watatu (3) akiwemo mshambuliaji wa kikosi hicho Josef Martinez, Victor Ulloa na Jak LaCava. Mshambuliaji Martinez hakuwa sehemu ya kikosi kilichocheza michezo miwili ya mwisho ya Ligi ya MLS msimu huu baada ya kocha Tata Martino kuthibitisha nyota huyo hayupo kwenye mipango yake msimu ujao.
Hii itakuwa njia rahisi kwa Suarez kujiunga na kikosi cha Inter Miami ambaye amethibitisha kuwa ataondoka mwishoni mwa msimu huu kwenye kikosi cha Gremio baada ya msimu huu wa Ligi kuu nchini Brazil (Seria A) kutamatika mwezi December. Msimu wa kawaida wa MLS utaanza kutimua vumbi mwezi wa pili mwakani.
Maamuzi ya Inter Miami kuachana na Martinez yataigharimu takribani $ 4.4 million (£3.5m) ambacho watakitumia kumlipa nyota kama sehemu ya mshahara wake. Kwa upande mwingine Suarez anapokea kiasi kinachokadiriwa kuwa ni $4.5 million (£3.6m) kwa mwaka akiwa na Gremio. Kama Suarez atajiunga na kikosi cha Inter Miami atalipwa kiasi kidogo kulinganisha na kile anachokipokea Gremio, lakini atapokea kiasi kikubwa cha pesa za udhamini na matangazo.
Suarez ana magoli tisa (9) na pasi za mwisho saba (7) kwenye michezo 24 ya ligi ya Serie A, Jumamosi hii atashuka dimbani na kikosi chake kuikabili klabu ya America-MG.