Kocha wa KMC Abdihamid Moalin amewaita mashabiki wa timu yake kuja kwa wingi kuwatia nguvu kwenye mchezo wa leo dhidi ya Wajelajela, Tanzania Prisons kwenye dimba la Uhuru, Dar es Salaam.
Mashabiki ni wachezaji wa 12 na wana nafasi kubwa sana kwenye kufanya timu yetu kufanya matokeo. Wamekuwa wakifanya hivyo kwenye michezo mingi na sisi tumejitahidi kupambana kwa ajili yao, iwe hapa nyumbani au ugenini.
Tunaomba waje kwa wingi pia kwenye mchezo wetu huu kwakuwa tunahitaji nguvu yao ili tuweze kupata alama 3 muhimu sana kwenye ligi hii.
Aidha katika upande mwingine, Moalin amesema kuwa mechi itakuwa ngumu na haitoiangalia kwa jicho la kawaida kama wengine wanavyodhani kwa kuwa ni mechi ngumu hata kihistoria.
Sitojali wanapitia mazingira gani kwa sasa, na siendi nikiwazia hilo hata kidogo. Unaweza ukaingia na mawazo kuwa hawapo kwenye wakati mzuri sasa hivi halafu ukakutana na kitu tofauti kabisa. Hivyo ntaingia na nguvu kubwa na nikiwa makini sana.
Uzuri nina kikosi kipana na wachezaji wote wapo tayari kutumika, maana ligi inavyoenda kila baada ya siku 2 kuna mechi hivyo inahitaji watu wote kuwa tayari na wapo tayari.
KMC watakuwa nyumbani leo wakiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu ya 0-0 na Tabora United wakimenyana na Tanzania Prisons ambayo nayo imetoka kutoka sare ya 1-1 na JKT Tanzania.