Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Roberto Oliveira amesema kuwa kikosi chake kipo tayari na kina ari nzuri kueleke mchezo wao dhidi ya Ihefu hapo kesho. Ameyasema hayo akiwa anazungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo wa ligi kuu ya NBC.
Kocha Robertinho amesema kuwa wanaiheshimu sana Ihefu lakini wao kama klabu malengo yao ni kushinda kila mchezo ulio mbele yao na hivyo lengo kuu siku ya kesho ni kucheza vizuri, kucheza kwenye msingi wao wa siku zote ili kumnyima nafasi mpinzani na kushinda mchezo huo muhimu.
Nini mpango wetu wa kesho? Mpango ni kucheza kwa vizuri na kucheza kwa nguvu, kumnyima nafasi mpinzani, ndio mpango wetu. Msingi pia ni kucheza vizuri na kutumia vipaji na uwezo tuliokuwa nao. Tuna vipaji vingi sana na wote wako tayari kwa mchezo huo. Nimewatizama wapinzani wetu, wana timu nzuri lakini nafikri sisi ni timu bora zaidi na tuna ari nzuri, tupo kwenye wakati mzuri na tunataka matokeo mazuri kwenye mchezo huo.
Kwa upande wa wachezaji kiungo mshambuliaji Shabani Idd Chilunda amesema kuwa wachezaji wapo tayari kupambana mengine yote yaliyopita yamepita.
Sasa hivi kuna wachezaji wapya, kwao na hata kwetu hivyo utakuwa mchezo mpya na mgumu. Sisi tunajiangalia msimu huu tulivyoanza na wao wanavyocheza. Sisi tumewaangalia na tunaamini na wao wametuangalia lakini sisi cha msingi tunataka alama tatu
Simba SC na Ihefu SC wanakutana kwa mara ya kwanza msimu huu katika uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 28, 2023 majira ya Saa 1:00 Usiku.