NBC Premier League

DODOMA JIJI YABISHA HODI 4 BORA, PRISONS, GEITA GOLD NGOMA NGUMU

Published on

Dodoma Jiji wanachukua alama zote 3 mbele ya maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex na kufikisha alama 12, alama 1 zaidi ya wapinzani wao wa leo na kusogea hadi hadi nafasi ya 4 ya msimamo wa ligi kuu wakimmshusha KMC.

JKT Tanzania wakicheza na mfumo wa 4-2-3-1 ni kama walianzia walipoishia kwenye mchezo uliopita wakishinda 1-0. Waliuanza mchezo kwa kasi na dakika ya 9 tu ya mchezo walitengeneza nafasi nzuri ya bao kutokea upande wa kulia, krosi ya George Amani Wawa ilishindwa kumaliziwa na Maka Edward.

Dakika ya 14 tena George Wawa alipiga tena krosi nzuri ya chinichini lakini Najim Magulu aliupaisha mpira huo. Nafasi nyingine ya wazi wakipoteza.

Ilimmlazimu Daniel Mgore kuwa mchezoni muda wote wa kipindi hiki cha kwanza kwani JKT walipeleka sana mashambuliz golini kwake, dakika ya 40 alipigiwa shuti kali na David Brayson lakini alifanikiwa kuokoa na kuwa kona.

Anderson Kimweri alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 43 baada ya kutishia kummpiga kijana muokota mipira.

Pamoja na kulisakama lango la Dodoma Jiji kwa muda mrefu bado hawakuweza kuwa an utulivu na kuandika bao. Upande wa kushoto wa Dodoma Jiji aliokuwa akicheza Emmanuel Martinnulionekana kama ndio njia kuu ya JKT kutengeneza mashambulizi. Martin ni winga kiuasilia na kukubaliana na wachezaji wawili wenye kasi, George Wawa na Sixtus Sabilo kulimmpa wakati mgumu.

Mapumziko JKT Tanzania 0-0 Dodoma Jiji.

Kipindi cha pili kilianza taratibu, kila timu ikiwa na tahadhari kubwa. Dakika ya 49 Dodoma Jiji walifanya mabadiliko kuongeza kasi ya mashambulizi, kwa kummtoa Raizin Hafidh na kumuingiza Zidane Sereri.

Dodoma walionekana kuchangamka sana kipindi hiki cha pili wakipanga mashambulizi yao vizuri. Dakika ya 52 Hassan Mwaterema alifanyiwa madhambi akiwa analielekea lango la wapinzani lakini Hassan Nassor alichukua kadi ya njano kwa ajili ya timu.

Hassan Dilunga alipiga shuti kali kuelekea golini  kwa Dodoma Jiji dakika ya 62 lakini alimmkuta Daniel Mgore yuko imara langoni. Dilunga alipata maumivu kwenye shambulio hili na kushindwa kuendelea na mchezo  nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla. Dakika hizi hizi pia Dodoma Jiji waliwaingiza Paul Peter Kasaunda na Mwana Kibuta David, nafasi za Emmanuel Martin na Salmin Hozza.

Haikummchukua muda Paul Peter kummfanya Melis Medo kuingia uwanjani kushangilia bao lake lililommfanya atokwe machozi. Dakika ya 71, alijitengenezea nafasi mwenyewe na Shuti kali la chini chini likammshinda golikipa Ismail Saleh na kuiandikia goli la uongozi timu yake. Goli stahili kabisa kwa namna Dodoma walivyokimiliki kipindi cha pili.

Kutokuwepo kwa Hassan Dilunga uwanjani ni kama palivuruga zaidi mpango kazi wa Malale Hamsini, kiungo kikonekana kuelemewa. Bado Ndemla hakuweza kufanya kama alichokuwa akikifanya Dilunga. Licha ya kuingia Danny Lyanga bado hapakuonekana kuwa na uhai kuanzia eneo la kiungo ushambuliaji hadi eneo la kumalizia. Pengine pia watajutia nafasi walizozipoteza kipindi cha kwanza.

Dodoma waliamua kuumaliza mchezo kwa kukubali kukaa na mpira hata wakiwa kwenye eneo lao, kila JKT walipojaribu kufurukuta aliwakuta wapinzani wao wako imara kiulinzi. Kazi nzuri ya Augustino Nsata na Jerome Nason. Dakika za mwisho anatolewa mshambuliaji Hassan mwaterema na kumuingiza mlinzi Adeyum Saleh.

Mpaka muamuzi Ally Mnyupe ana puliza kipyenga cha mwisho, JKT Tanzania 0-1 Dodoma Jiji.

Kwingineko, Jijini Mbeya, Tanzania Prisons na Geita Gold wameendelea kuwa na msimu wa tabu baada ya kutoka suluhu ya 0-0 leo hii kwenye dimba la sokoine jijini Mbeya na kuzidi kujiwekea mazingira magumu. Prisons wanafikisha alama 7 na kusogea hadi nafasi ya 12 na Geita Gold wafikisha alam zao 6 wakisogea nafasi 1 hadi ya 15 kutoka 16.

Kwenye mchezo ambao ulikuwa na nafasi chache sana, timu zote hazikuonyesha uhai hasa kwenye eneo la ushambuliaji. Lakini pia hutoacha kusifu kazi nzuri za magolikipa wote wawili na safu za ulinzi.

Hakuna mbabe Sokoine.

Popular Posts

Exit mobile version