International Football

TUKO TAYARI KUWAKABILI BOTSWANA – SHIME

Published on

Kocha wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Bakari Shime amesema kuwa maandalizi yote ya muhimu kuelekea mchezo wa kesho wa marudiano wa kuwania kufuzu mashindano ya Olimpiki 2024 dhidi ya Botswana, jijini Gaborone yamekamilika kwa asilimia 100.

Tangu timu imewasili hapa jijini Gaborone, baada ya safari ndefu ya uchovu wa hapa na pale, walifanya mazoezi gym ya kurudisha miili kwenye hali yake ya kawaida kabla ya kufanya mazoezi kidogo jioni uwanjani. Wachezaji wote wako vizuri na wana ari ya mchezo.

Akizungumzia wachezaji wanaoweza kukosekana kwenye mchezo huo alisema kuwa wapo baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi tangu wakiwa Tanzania lakini kwa namna anavyowaona wakiendelea anaamini watakuwa tayari kwa ajili ya mchezo.

 Mwalimu Shime pia alisema kuwa anafahamu wana mchezo mgumu bado licha ya kuwa mbele kwa kuwa Botswana sio timu mbaya, wana uwezo mzuri sana na pia watahitaji matokeo ili na wao wafufue matumaini yao ya kushiriki Olimpiki.

Tunawajua vizuri Botswana tumecheza nao sio chini ya mara nne. Hata wao wanatujua vizuri ndio maana mechi yetu mliiona ilikuwa na upinzani. Tunaomba Mungu wachezaji wazidi kuimarika, waamke salama na kuweza kwenda kupambana kupata ushindi.

Twiga Stars walipata ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza nyumbani wa mzunguko wa pili  kwenye dimba la Azam Complex. Wakifanikiwa kuwatoa Botswana, basi wataingia mzunguko wa tatu wenye timu 8 utakaopigwa kwenye mtindo wa nyumbani na ugenini kabla ya kupata nyingine 4 zitazogombea nafasi 2 za dhahabu kuiwakilisha Afrika kwenye mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika Mwakani 2024 kati ya Julai 25-Agosti 10, jijini Paris, Ufaransa.

Mchezo wa marudiano utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana, jijni Gaborone, kesho tarehe 31/10/2023, saa 12 Jioni.

Popular Posts

Exit mobile version