NBC Premier League

TUMEJIPANGA KWELI KWELI – AHMED ALLY

Published on

Meneja wa habari na mawasiliano wa Klabu ya soka ya Simba, Ahmed Ally leo amezungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wao wa ligi kuu dhidi Yanga utakaopigwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya tarehe 5/11/2023.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Ahmed alisema kuwa wamejipanga vizuri kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mchezo huo kwakuwa ni mchezo muhimu kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Azam hawezi kutufikia tena, mpinzani aliyebaki ni Yanga ambaye na yeye tunataka kumfunga na kumpita kwa alama sita. Ni mechi ambayo tunaitaka kweli kweli, kuanzia kwa mashabiki, benchi la ufundi, wachezaji na viongozi ndio hata hatulali. Ni mechi ambayo Wanasimba inabidi tujitoe muhanga ili kupata ushindi. Tukishinda siku hiyo shughuli itakuwa imeisha, itabaki shughuli ya kukamilisha ratiba ya msimu

Aidha, alisema kuwa timu inatarajia kuingia kambini mapema kwa ajili ya kujiandaa na mchezo kutokana na ukubwa wake na mahitaji yake

Kikosi kitaingia kambini kesho Jumanne, kwa kawaida mechi za ndani huwa tunaingia siku tatu kabla ya mchezo lakini hii tunawahi. Tumeutolea macho mchezo huu kuhakikisha tunapata ushindi.

Katika upande mwingine, aliendelea kuwaita mashabiki kwenye mchezo huo ikiwa pamoja na kuweka wazi viingilio vya mchezo huo na kufungua hamasa mpaka siku ya mchezo wenyewe.

Sisi hatuna jambo dogo hivyo tutafanya hamasa, ni mchezo wetu, tutautangaza tutakavyo tunajua watu watakuja lakini lazima tuichangamshe. Tutakuwa na wiki ya mchakamchaka, hivyo wa kuaga kwao aage kabisa kuwa atarudi Jumatatu ya Novemba 6, 2023.

Siku ya Ijumaa tutakuwa na biryan la derby. Bado tunaangalia eneo la kufanyia.

Viingilio vitakuwa kama ifauatvyo; Mzunguko – Tsh. 5,000, Machungwa – Tsh. 10,000, VIP C – Tsh. 20,000, VIP B – Tsh. 30,000, VIP A – Tsh. 40,000 na Platinum – Tsh. 150,000.

Ahmed Ally pia hakuacha kuzungumzia ubora wa wapinzani wao na ugumu wa mchezo huo akisema kuwa wana timu bora na wachezaji wanaojituma. Hivyo haitokuwa mechi nyepesi lakini wamejiandaa vilivyo kushinda  mchezo huo.

Popular Posts

Exit mobile version