Taarifa zinazomuhusisha mshambuliaji raia wa Sweden na mchezaji wa zamani wa vilabu vya Ajax, Juventus, Inter Milan, Barcelona, PSG, Man United, La Galaxy na AC Milan Kurudi katika viunga vya AC milan nchini Italia zimezidi kushika kasi.
Kwa zaidi ya miezi miwili wasimamizi wa Milan wamekuwa wakizungumza na kutafuta suluhisho, huku pia mikutano ya mara kwa mara ikiwa imefanyika. Ibrahimovic tayari amekutana na Gerry Cardinale ambaye ni mmiliki wa Milan mara mbili, kisha Mkurugenzi Mtendaji Giorgio Furlani na Rais Paolo Scaroni kwa nyakati tofauti katika wiki zilizopita. Milan wanaamini kurejea kwake itakuwa muhimu ili aweze kusaidiana na kocha Stefano Pioli.
Hata hivyo, Zlatan bado hajatoa tamko lolote huku dalili zikionesha bado hajaridhishwa na mpango huo. Ukweli unabaki kuwa aliacha kucheza miezi mitano tu iliyopita na bado anataka kufurahia mapumziko baada ya kazi ndefu na yenye mafanikio. Zlatan mwenye umri wa miaka 41 anatathmini kwa utulivu nini cha kufanya katika siku zijazo, pia kwa sababu ana shughuli nyingi za ujasiriamali ambazo kwa sasa anazifanya. Milan hawakuweka ‘ukomo wa muda’ kwa Ibra, lakini wanatumai kupokea jibu kutoka kwake haraka iwezekanavyo.