Serikali ya Colombia mapema jana (Alhamis) ilitoa taarifa kuwa tayari imewafahamu watekaji wa familia ya nyota kiungo mshambuliaji wa klabu ya Liverpool, Luiz Diaz ambao walimteka Baba yake pamoja na Mama yake ni kikundi cha waasi cha jeshi la ukombozi wa Taifa (ELN).
Baada ya taarifa hiyo ya Serikali leo mwakilishi wa kikundi cha ELN ametoa waraka unaosema kuwa wako mbioni kumuachilia Baba mzazi wa Luiz Diaz ambaye walimteka.
Kwenye taarifa iliyotolewa kwa njia ya video mwakilishi wa kundi la ELN Juan Carlos Culler amesema Luis Manuel ataachiliwa haraka iwezekanavyo kitu ambacho ni maendeleo makubwa kwenye kesi hiyo. ELN ilianzishwa mwaka 1964, na ndicho kikundi cha kigaidi chenye nguvu zaidi nchini Colombia.
Mwezi Agosti mwaka huu serikali ya Colombia na kikundi hicho cha ELN waliingia makubaliano ya amani ya kusitisha mapigano na uharifu uliokuwa ukifanywa na kikundi hicho. Waziri wa mambo ya ndani wa Colombia Luis Fernando Velasco amesema jana Alhamis kuwa makubaliano ya usitishaji wa mapigano na uharifu yamevunjwa baada ya kikundi cha ELN kufanya utekaji huo.
Baba yake Diaz alitekwa jumapili iliyopita pamoja na Mama yake, Cilenis Marulanda na wanaume waliokuwa kwenye pikipiki. Marulanda aliachiliwa masaa machache baadae lakini Luis Manuel hajaonekana tangu alipotekwa, hofu ikiwa huenda amevushwa mpaka hadi nchi ya Venezuela.
Luiz Diaz amekosekana katika michezo miwili iliyopita ya Liverpool wakati ambao akishughulikia upatikanaji wa Baba yake.