Mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa Barani Afrika klabu ya FAR Rabat kutoka Morocco wameanza vibaya mashindano baada ya kichapo cha goli 1-2 kutoka kwa Ampem Darkoa Ladies.
Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa Wanawake imeendelea hapo jana November 6 kwa michezo miwili ya kundi B kuchezwa. Bingwa mtetezi FAR Rabat ya Morocco iliingia dimbani kuikabili Ampem Darkoa Ladies ya nchini Ghana katika uwanja wa Stade Laurent Pokou, San Pedro. FAR Rabat ilikubali kichapo cha kwanza cha mashindano haya cha magoli 1-2.
Alikuwa ni Najat Badri (35) aliyeipatia timu yake ya FAR Rabat goli la kuongoza dakika ya 14 ya mchezo baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Nouhaila Benzina, hadi timu zinaenda mapumziko FAR Rabat walikuwa wanaongoza 1-0.
Mapema dakika ya 57 vijana wa Ampem Darkoa Ladies walisawazisha goli hilo kupitia kwa nyota wake mshambuliaji Comfort Yeboah (16) na baadae dakika ya 61 vijana wa Ampem Darkoa Ladies walihitimisha karamu ya magoli kwa goli la kujifunga la Nouhaila Benzina (25).
Mchezo mwingine uliopigwa usiku kuanzia saa tano ulikuwa Huracanes dhidi ya AS de Mande ya Mali na Huracanes ya Equatorial Guinea uliomalizika kwa sare ya 1-1, mchezo ambao pia ulipigwa katika dimba la Stade Laurent Pokou, San Pedro.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyokuwa imeliona lango la mwenzake. Dakika ya 66 Elena Nkuandum (23) aliiandikia timu yake ya Huracanes goli la uongozi kwa mkwaju wa Penalty kabla ya Fatoumata Diarra (37) kuisawazishia timu yake dakika ya 72 ya mchezo baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Oumou Kone (23).