Top Story

SIMBA WAENDE WAKARIPOTI TAKUKURU.

Simbachawene amesema hayo leo wakati akijibu swali la Nyongeza la Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kupambana na rushwa michezoni.

Published on

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameiomba klabu ya Simba kama imebaini vitendo vya rushwa katika mchezo wake dhidi ya Yanga SC uliochezwa November 5, 2023 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam itoe taarifa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Manispaa ya Temeke ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Rushwa michezon haikubaliki, kama mchezo una viashiria vyovyote vya rushwa, niwaombe sana klabu ya Simba, waende wakaripoti ofisi ya Takukuru Temeke, kama zile tano (5) zimetokana na rushwa.

Waziri, Simba chawene akizungumza leo Bungeni, Dodoma.

Simbachawene amesema hayo leo wakati akijibu swali la Nyongeza la Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kupambana na rushwa michezoni akitolewa mfano baadhi ya Wachezaji wa Simba kusimamishwa kwa madai ya kuwepo kwa viashiria vya rushwa katika mchezo huo.

Awali akijibu Swali hilo Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema Wizara kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekua ikipinga vitendo vya rushwa michezoni ambapo kwa kushirikiana na TAKUKURU wamekua wakitoa Elimu kuhusu suala hilo na kwamba tayari wameaanzisha Kampeni inayoitwa “Kataa upangaji wa matokeo, linda hadhi ya mpira wa miguu” ambayo inaendelea kuleta matokeo mazuri pia kushirikiana na Wadau wengine wa michezo vikiwemo vilabu husika kupinga vitendo hivyo.

Mwanzoni mwa msimu huu TFF kwa kushirikiana na Takukuru, ilianzisha mradi ambao unaitwa ‘Kataa upangaji wa matokeo, linda hadhi ya mpira wa miguu’, na nafahamu hili sio swala ambalo linaweza kutatuliwa siku moja, malalamiko ni mengi lakini tunafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu, kupunguza au kuondoa kabisa viashiria na vitendo vya rushwa kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

Kwa kuthibitisha hilo Takukuru wameshaanza kukaa na wadau mbalimbali kuhakikisha wanatoa elimu na kuwaelimisha kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa vitendo vya rushwa katika michezo na kupanga matokeo vikibainika.

Takukuru imeshakaa na chama cha wachezaji wa zamani, imeshakaa na chama cha waamuzi, vilabu vya Ligi kuu, taasisi za fedha, kampuni za michezo ya kubashiri na wadau wengine mbalimbali, na sisi jambo hili hatutaki kuliona likieendelea chini ya usimamizi wetu na tunafanya kila lililopo ndani ya uwezo wetu ikiwemo kushirikiana na taasisi nyingine za kupinga mambo yasiyofaa michezoni kama takukuru ili kuhakikisha yanakomeshwa kabisa.

Waziri, Hamis Mwinjuma.

Popular Posts

Exit mobile version