Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amesema hakuna kikwazo kwa timu yoyote ya Ligi Kuu kuchagua Uwanja wa Nyumbani Visiwani Zanzibar.
Mwijuma amesema timu zina uhuru wa kuchagua uwanja wowote wa Jamhuri ya Muungano bila vikwazo vyovyote bila kuathiri kanuni na miongozo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Tanzania na Shirikisho la soka Zanzibar (ZFF).
Naibu Waziri huyo amesema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati akijibu swali la mbunge Mussa Omar Salim wa Gando aliyeuliza,
Kwa nini baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya Tanzania zisichezwe kwenye Viwanja vya Gombani na Amaan vilivyopo Pemba na Unguja.
Mussa Omar Salim, Mbunge wa Gando, Visiwani Zanzibar.
Endapo timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu itawiwa kutumia Uwanja vya Gombani na Amaan Zanzibar kama Uwanja wa nyumbani hakutakuwa na kikwazo chochote ikiwa timu itakidhi makubaliano na uongozi unaosimamia taratibu na matumizi ya uwanja husika bila kuathiri Kanuni na miongozo ya TFF na Bodi ya Ligi Tanzania.
Hamis Mwinjuma, Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Kanuni ya 9:7 ya Bodi ya Ligi inaruhusu timu ya Ligi Kuu kuchagua viwanja vingine miongoni mwa vile visivyotumika katika mchezo wa Ligi Kuu kwa michezo yake miwili tu ya nyumbani na kuwasilisha uteuzi wake siku ishirini na moja kabla ya mchezo husika unaokusudiwa kuchezwa kwenye uwanja ulioteuliwa.