Klabu ya Young Africans mapema leo imechapisha bango barabarani linaloonyesha matokeo ya ushindi waliyoyapata katika mchezo wa Ligi kuu dhidi ya mahasimu wao wakubwa klabu ya Simba. Bango hilo limechapishwa katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi Jijini Dar Es Salaam, likionyesha matokeo ya mchezo ambayo yalikuwa ni 1-5 na majina ya wafungaji wa magoli hayo.
Hii inaonyesha namna ambavyo timu hii ilifurahia zaidi kupata matokeo hayo makubwa mbele ya mtani wake wa jadi klabu ya Simba, Yanga haijawahi kupata matokeo kama hayo na imekuwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake kuifunga klabu ya Simba magoli matano katika mchezo mmoja.
Swala hili limezua hisia kubwa sana kwa mashabiki wa soka nchini wengi wakitaja kama sehemu ya kuwatangaza zaidi wadhamini wake lakini pia sehemu ya kudumisha dhana ya utani katika soka la Tanzania kwa timu hizi mbili.
Hadi hivi sasa klabu ya Young Africans inatajwa kufanikiwa zaidi katika kuwatangaza wadhamini wake kupitia matokeo haya ambayo wameyapata mbele ya mtani wake wa jadi klabu ya Simba, kupitia bango hili watu wengi wameliona na limesambaa zaidi katika mitandao ya kijamii, kitu ambacho kinaweza kuwavutia zaidi wadhamini mbalimbali kujitokeza kuidhamini klabu hiyo.
Lengo kuwakumbusha watani zetu kilichotokea November 5,… Tunaweka mabango Dar Es Salaam yote, leo mpaka kufika jioni tutakuwa na video ambayo itakuwa inacheza kwenye Billboard matukio ya magoli yote yale matano.
Afisa habari na mawasiliano wa klabu ya Yanga, Ahmed Ally, akizungumza baada ya kuweka mabango katika viunga vya Jiji ya Dar Es Salaam.
Kimpira mmefaulu kwa maana ya utani wa jadi hii ni kama Manchester City walipomnasa Tevez kutoka Manchester United wakatia bango katikati ya Jiji, Fergie aliumia sana, yalimtoka maneno mengi sana, kibiashara pia mmefaulu wadhamini wenu watapata value zaidi kwakuwa ishakuwa Talk of the Country, kazi nzuri kwenu ila ipo siku Tutalipa hii.
Shabiki mmoja wa simba aliandika.
Hii timu sasa inashangaza Dunia, yaani hamuamini kama mlitufunga goli tano huu ni zaidi ya ushamba.
Shabiki mwingine wa Simba aliandika.
Ni wakati mwafaka sasa tuhamie kwenye goli 7 au wakati mwingine mtani akileta dharau tumfunge 10.
Shabiki mmoja wa Young Africans aliandika.
Sema Yanga tukianza kero huwa hatumalizi.
Shabiki mwingine wa Yanga aliandika.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa timu kutoka Tanzania kuweka bango kubwa katikati mwa barabara baada ya kupata matokeo ya ushindi katika mchezo wa Ligi. Young Africans ilianza na kunywa supu yalipo maskani ya klabu hiyo baada ya ushindi wa timu hiyo.
Hii aio mara ya kwanza kwa Young Africans kufanya matukio kwa mara ya kwanza, ilianza na zoezi la kuwapokea wachezaji wapya wanaosajiliwa na klabu hiyo Airport, baadae wakafanya parade kubwa ya ubingwa iliyotikisa Afrika na kuweka pia sherehe za za kumaliza nafasi ya pili kwa kupatiwa medali katika mashindano ya shirikisho Barani Afrika.