Taarifa za awali kutoka katika viunga vya klabu ya Tabora United inayoshiriki Ligi kuu kandanda Tanzania Bara zilikuwa zinadai kuwa, Wachezaji wazawa wa klabu hiyo, jana waligomea kufanya mazoezi na timu kwasababu hawajalipwa mishahara yao wakati wachezaji wa kigeni wao wakipata stahiki zao.
Kwa mujibu wa taarifa zilidai kuwa jana Tabora United ilikuwa imepanga kufanya mazoezi asubuhi na jioni lakini baada ya mgomo huo, mazoezi hayakufanyika na ikapelekea wachezaji wa kigeni kufanya mazoezi Barabarani [Road Work].
Dauda Sports ikalazimika kumtafuta Afisa habari wa klabu ya Tabora United Pendo Lema ambaye amethibitisha kuwa ni kweli baadhi ya wachezaji hawapo kambini kwasababu wana ruhusa maalumu ya mapumziko na sio kwamba hawajalipwa stahiki zao.
Jana ni kweli hatujafanya mazoezi, juzi tulifanya mazoezi, tulikuwa na mapumziko, kwahiyo kuna baadhi ya wachezaji walipewa mapumziko ya siku tano,.. Kama unavyojua sasa hivi kuna kipindi kirefu sana cha mapumziko cha kupisha mashindano ya FIFA, kwahiyo sisi tuliwapa mapumziko wachezaji wetu baadhi lakini wengine bado wapo.
Wa kigeni hawawezi kusafiri kwenda umbali mrefu, kama unavyojua sisi tuna wachezaji wametoka nchi za mbali, wachezaji wametoka Nigeria, Congo wengi kwahiyo sisi tusinge wapa ruhusa ya kwenda kwao kusalimia ni mbali sana, na sisi tuliowapa mapumziko wengi sana ni Watanzania.
Wachezaji wameshalipwa, tena wamelipwa tangu tulipotoka Geita, kuna wengine ambao ni baadhi, kulikuwa kuna matatizo ya hizi kadi, kuna wengine wamrtokea nje kwahiyo kadi zao zinasumbua, kama huyu Didier ambaye tulimsajili kutoka Mbeya City, huyu kibali chake kina sumbua sana, huyu ndiye anayetudai wengine wote wapo vizuri.
Pendo Lema, Afisa habari na mawasiliano wa klabu ya Tabora United.
Pendo ameweka wazi kuwa kikosi kitarejea kambini hivi karibuni baada ya likizo ya wachezaji kumalizika ili kujiandaa na michezo ijayo ya Ligi kuu kandanda Tanzania Bara. Msikilize hapa chini akieleza.