FIFA World Cup

STARS YAWASILI NCHINI YAPOKEA MILLION 10 ZA RAIS.

Published on

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kimewasili nchini Tanzania kikitokea nchini Morocco ambako kilikuwa na mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya Niger, uliomalizika kwa ushindi wa goli 1-0.

Stars ilipatiwa ndege na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyowapeleka na kuwarudisha nchini. Mara baada ya kutua nchini kikosi hicho kitapata mapumziko mafupi na kesho kitaendelea na mazoezi ili kujiandaa na mchezo wa Jumanne dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco.

Baada ya kutua nchini walipokelewa na katibu wa Utamaduni Sanaa na Michezo Gerson Msigwa ambaye licha ya mambo mengi aliyoyasema kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimkabidhi nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta kiasi cha Million 10 aliyoiahidi Rais kila timu hiyo inapopata goli katika mchezo itakayoshinda.

Msigwa pia amewaambia watanzania kuwa hakuna haja ya kusalia nyumbani siku ya Jumanne katika mchezo dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco kwani Mh. Rais amenunua tiketi zote za mzunguko hivyo jukumu lililosalia ni kwa Watanzania kwenda kuujaza uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mheshimiwa Rais amefurahi sana kwa ushindi wa jana na anawatakia kila lakheri kwenye pambano lenu dhidi ya Morocco tarehe 21, anawatakia kila lakheri mshinde tujiweke kwenye nafasi nzuri ya kucheza kombe la Dunia.

Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba kwenye safari ya Taifa Stars kila goli atakuwa anatoa Million Kumi kwa pambano mnaloshida.

Nimetumwa niwakabidhi shilling Million 10 alizozitoa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hii ni chachu ya kuwatia moyo, japo Rais hatakuja uwanjani ameamua kulipia tiketi za mzunguko za uwanja wote wa Benjamin Mkapa tarehe 21, watanzania kazi yenu ni kuja uwanjani kuishangilia timu.

Hii tumeamua kuiita OPARESHENI SAMIA KOMBE LA DUNIA, tumeianza jana, tunataka ushindi tarehe 21, tushinde na mechi zinazofata, tunataka tucheze kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Mkapambane mkijua mabegani mwenu mmebeba watanzania million 62.

Watanzania hatuna sababu ya kutokuwepo uwanjani Jumanne , Twende tukajae Benjamin Mkapa, wale jamaa tuwafunge kwa kidedea, yaani sisi tushangilie hadi jamaa waachie goli.

Katibu mkuu wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo akizungumza akiwa uwanja wa ndege kuwapokea wachezaji wa Taifa Stars.

Nahodha wa kikosi cha Stars Mbwana Ally Samatta amemshukuri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa ndege iliyowarahisishia safari yao na kuwataka watanzania wajitokeze kwa wingi kuwapa nguvu katika mchezo huo wa jumanne.

Ningependa kumshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia, kwa motisha imefika.

Cha pili kikubwa ambacho ametusaidia kwa kiwango kikubwa ni kutupa usafiri wa kwenda nchini Morocco kwaajili ya mechi dhidi ya Niger.

Ukimuuliza mtu yoyote ambaye alikuwa kwenye safari atakuambia umbali wa safari jinsi ulivyokuwa, kama wachezaji tulikuwa tunafikiria ni kiasi gani tungepata tabu kama tungesafiri na ndege ya kawaida.

Lakini kwa upendo wake ametupatia ndege ambayo imetusafirisha vizuri, na ninauhakika naweza kusema kwa asilimia 50 amechangia matokeo ya mechi ya jana kwasababu wachezaji walienda vizuri kwa amani na walikuwa na furaha.

Nina waomba watanzania siki ya jumanne waje tushiriki kwenye hii mechi pamoja kwasababu hii ni timu ya Taifa ya Tanzania na ni ya watanzania wote.

Mbwana Samatta, Nahodha wa Taifa Stars akizungumza mara baada ya kikosi hicho kuwasili nchini.

Taifa Stars itashuka dimbani kuikabili Morocco kesho kutwa Jumanne katika uwanja wa Benjamin Mkapa majira ya saa nne usiku (22:00) kwa saa za Afrika Mashariki. Stars ipo nafasi ya pili ya msimamo wa Kundi E ikiwa na alama tatu nyuma ya Zambia zikitofautiana magoli. Kundi E lina timu za Tanzania, Niger, Congo Brazzaville na Morocco.

Eritrea imejitoa katika mashindano hayo kutokana na hali ya kiusalama wakihofia wachezaji wao kutoroka kwenye kambi ya timu hiyo ambayo ilikuwa imepangwa kuwekwa nchini Morocco hivyo kundi E linasalia na timu tano pekee.

Kinara wa kundi hili atafuzu moja kwa moja kwenda kushiriki fainali za kombe la Dunia mwaka 2026 na timu itakayomaliza nafasi ya pili italazimika kucheza na timu zingine ili iweze kufuzu. Afrika itawakilishwa na timu tisa za moja kwa moja.

Popular Posts

Exit mobile version