Timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania chini ya miaka 20 “Tanzanite” imeondolewa kwenye mchakato wa kufuzu fainali za kombe la Dunia la 2024 litakalofanyika nchini Colombia baada ya kukubali kipigo cha goli 2-1 ugenini dhidi ya timu ya Taifa ya Nigeria.
Mchezo huo hadi mapumziko timu zote mbili zilikuwa zimetoshana nguvu ya kufungana goli 1-1 na mapema kipindi cha pili timu ya Taifa ya Nigeria iliongeza goli la pili na la ushindi kwenye mchezo huo, hivyo hadi kipyenga kinapulizwa katika uwanja wa Moshood Abiola Nigeri 2-1 Tanzanite.
Matokeo hayo sasa yanaishuhudia Tanzanite ikiondoshwa kwa jumla ya magoli 3-2 baada ya mchezo wa awali uliopigwa katika dimba la Azam Complex, Dar Es Salaam kumalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1.
Hata hivyo timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake haijawahi kupata matokeo mazuri mbele ya timu ya Taifa ya Nigeria kwani hadi kufikia leo katika michezo minne (4) iliyopita haijawahi kupata ushindi wowote, imeambulia sare moja (1) na kipigo mara tatu (3). Huku ikifungwa magoli 12 na ikifunga magoli mawili (2) pekee.