FIFA World Cup

STARS IPO KAMILI KUIKABILI MOROCCO.

Published on

22:00 Tanzania vs Morocco

UWANJA: Benjamin Mkapa

Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars inaendelea na maandalizi yake kuelekea mchezo wa pili dhidi ya Morocco wa hatua ya makundi wa kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Mexico pamoja na Canada.

Taifa Stars itashuka dimbani kesho saa nne kamili usiku (22:00) kuikabili timu ya Taifa ya Morocco katika uwanja wa Benjamin William Mkapa, Dar Es Salaam. Kuelekea katika mchezo huo kocha msaidizi wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania amesema maandalizi ya mechi dhidi ya Niger ni tofauti na maandalizi dhidi ya Morocco na mambo yote yamekamilika.

Kikosi ambacho tuko nacho baadhi ya wachezaji walikuwa majeruhi, baada ya hapo wakarudi kwenye kikosi, ikabidi tujiandae jinsi ya kucheza kupambana na Niger.

Kikubwa kilichopo tunaendelea kuangalia makosa wapi yalipo na maandalizi ya mechi ya Niger ni tofauti na mechi ya Morocco.

Kuna mbinu ambazo tutatumia kwenye mechi ya Morocco, hata wale wachezaji watakaopata nafasi katika kikosi cha kwanza watatumia hizo mbinu na watajituma na kujitolea na mchezo utakuwa mzuri.

Tunatumia vipaji na wachezaji ambao tunao, hatuwezi kutumia vipaji ambavyo hatuna na tunawatumia kwenye mfumo ambao tunacheza.

Kikubwa ni kuwaamini wachezaji tulionao, na kuwatengeneza vizuri maana hatuwezi kuruka hatua, lazima twende sawa na wachezaji tulionao.

Tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuwatumia ambao tuko nao ili tupate matokeo mazuri.

Fuad kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania.

Nyota wa timu ya Taifa ya Morocco na nahodha msaidizi wa timu hiyo Ashraf Hakimi amesema wamejipanga vyema kuelekea mchezo wa kesho na wamejiandaa vyema kukabiliana na kikosi kizima cha Taifa Stars akiwemo nahodha wa kikosi cha Stars Mbwana Ally Samatta.

Mpira wa miguu utabaki kuwa mpira wa miguu haijalishi unacheza ulaya au unacheza wapi lakini mpira wa miguu ni uleule, na ndio maana tumekuja mapema, ili kujiandaa vizuri, kuangalia mazingira ili kupata matokeo mazuri.

Kikosi chote cha Tanzania ni kizuri, nahodha wa timu Mbwana Samatta ni mzuri namjua na tumejipanga kupambana na kikosi kizima na lazima tuingie kwa makini ili tuweze kupata alama tatu turudi nazo nyumbani.

Ashraf Hakimi nahodha msaidizi wa timu ya Taifa ya Morocco.

Stars inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya Niger uliofanyika Jumamosi iliyopita nchini Morocco.

Morrocco bado haijacheza mchezo wowote hadi hivi sasa baada ya timu ya Taifa ya Eritrea kujitoa mashindanoni kwa hofu ya wachezaji wake kutoroka kwenye kambi ya timu hiyo ambayo ilipangwa kuwekwa nchini Morocco.

Katika michezo miwili ya mwisho ambayo timu hizi mbili (2) zimekutana, Tanzania imeshinda mara moja (1) na Morocco imeshinda mara moja (1).

24/03/2013 Tanzania 3-1 Morocco

08/06/2013 Morocco 2-1 Tanzania

Popular Posts

Exit mobile version