Baada ya Kamati ya Kusimamia na Kuendesha Ligi ya Bodi ya Ligi (TPLB) kutangaza kumfungia kiungo wa Yanga, Khalid Aucho kwa mechi tatu na kumlima faini ya Sh500,000 kwa kosa la utovu wa nidhamu, mabosi wa klabu hiyo wanadaiwa wapo kwenye mchakato wa kukata rufaa.
Aucho alikumbana na kibano hicho kutokana na kosa la kumpiga kiwiko nahodha wa Coastal Union, Ibrahim Ajibu Migomba katika mchezo namba 71 uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Akizungumza, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo alisema uongozi haujakubaliana na uamuzi huo wa kamati hiyo ya bodi ukiona kiungo huyo amehukumiwa mara mbili.
Gumbo alisema wanalazimika kukata rufaa kutokana na kuwa waliwahi kuiandikia barua Bodi ya Ligi siku za nyuma juu ya beki wa Simba, Henock Inonga aliyefanya kosa kama hilo, lakini walijibiwa mwamuzi alishachukua hatua ndani mchezo kwa kuonyeshwa kadi ya njano, ila safari hii Aucho hilo limesahaulika.