Ligi kuu ya Tanzania Bara inarejea tena leo baada ya mapumziko ya takribani wiki mbili kupisha dirisha la mechi za kimataifa za timu za taifa, kwa michezo miwili itakayopigwa majira ya saa 10 Jioni na Saa 1 Jioni.
Kwenye Dimba la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu, Geita Gold watakuwa wenyeji kuwakaribisha JKT Tanzania kwenye harakati zao za kujinasua kutoka upande wa chini kabisa wa msimamo wa ligi kuu.
Geita Gold wapo nafasi ya 15 wakiwa na alama 7 baada ya kucheza michezo 9 na wanahitaji sana alama 3 leo wakiwa nyumbani baada ya kuwa na mwenendo mbovu katika mechi zao za hivi karibuni wakishinda mechi 1 tu kati ya mechi zake 9. Geita Gold walitoka 0-0 dhidi ya Tabora United.
JKT Tanzania wapo kwenye nusu ya nzuri ya msimamo wa ligi, wakishika nafasi ya 6 wakiwa na alama 14 baada ya mechi zao 9 pia. Magoli ya Danny Lyanga na Najim Magulu dhidi yalitosha kuwapa ushindi wa 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Manungu kwenye mchezo wao wa mwisho. Mchezo huu utapigwa saa 10 Jioni.
Kwingineko kwenye uwanja wa Kaitaba, Kagera watawakaribisha KMC kwenye mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake kutokana na viwango vya wachezaji wa timu zote mbili lakini pia makocha wote, Mecky Mexime na Moalin wanapenda mifumo ya kucheza kwa kufungua uwanja.
Kagera Sugar wapo nafasi ya 8 wakiwa na alama 12 baada ya michezo 9 huku wakitoka kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwa magoli ya Obrey Chirwa na Cleophace Mkandala. Wapo kwenye kiwango kizuri kwenye mechi za hivi karibuni na wakianza kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani, watatamani kuendelea walipoishia.
KMC walikusanya alama nyingi sana hivi karibuni mpaka kuwaweka hapo walipo, nafasi ya 5 wakiwa na alama zao 15. Wakizungumzia malengo yao kila siku ni kumnaliza mingoni mwa timu 4 bora na kwa namna wanvyozichanga karata zao, mwanga unaonekana kwao, licha ya kupoteza 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji nyumbani lakini bado walicheza vizuri. Mchezo huu utapigwa majira ya saa 1 Jioni.