Nyota wa Timu ya Taifa ya Tanzania na klabu ya Shakhtar Donetsk, Novatus Dismas Miroshi amewaomba radhi mashabiki na wapenzi wa soka Tanzania kufuatia kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo wa jana dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco wakati timu yake ikipoteza kwa magoli 2-0.
Nipende kuwaomba radhi wapenda soka wote na wa Tanzania kwa kupata Cadi nyekundu lakini bado tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri.
Novatus Dismas, nyota wa Taifa Stars.
Miroshi alionyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 65 ya mchezo baada ya vurugu kati yake na nyota wa klabu ya Manchester United Sofyan Amrabat hivyo kumfanya atoke nje kwa kadi nyekundu. Kadi ya kwanza ya njano aliipata dakika ya pili tu ya mchezo aliposababisha Morocco kupata mkwaju wa penalty kwa kumchezea vibaya Amine Adli.
Novatus Dismas atakosekana kwenye mchezo mmoja pekee wa timu ya Taifa ya Tanzania wa kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za kombe la Dunia 2026. Mchezo unaofuata kwa Tanzania katika michuano hii ni dhidi ya Zambiaambao utapigwa mwezi wa sita mwakani [June, 2024].
Tanzania itakutana tena na timu ya Taifa ya Morocco katika michuano ya fainali za mataifa ya Afrika [AFCON2023] zitakazofanyika nchini Ivory Coast, Jumatano ya January 17, 2024.