Muda mchache baada ya kutoka taarifa za kufungiwa kufanya usajili na shirikisho la soka Duniani FIFA, kutokana na kutokuilipa klabu ya Teungueth ya Senegal, sehemu ya pesa ambazo klabu ya Simba ilizipata baada ya kumuuza nyota wake Pape Ousmane Sakho kwenda Quevilly Rouen Metropole ya Ufaransa, klabu hiyo ya msimbazi imetoa taarifa ikidai kuwa imekamilisha asilimia 50 ya malipo hayo na imebaki asilimia 15.
Klabu ya Simba inapenda kuujulisha Umma kuwa ilimuuza mchezaji Pape Ousmane Sakho kwa klabu ya Quevilly Rouen Metropole ya Ufaransa mwezi August 2023. Makubaliano ya malipo ni ya awamu mbili.
Malipo ya awamu ya kwanza (50%) yalilipwa October 2, 2023. Klabu ya Simba ilikuwa inasubiri awamu ya pili ili kuilipa asilimia 15 ya mauzo kwa klabu ya Teungueth ya Senegal.
Klabu ya Simba inakiri kuwa kulikuwa hakuna mawasiliano na klabu ya Teungueth ya Senegal yaliyopelekea kadhia hii. Hata hivyo, klabu ya Simba inapenda kuujulisha Umma kuwa iko mbioni kukamilisha malipo hayo hivi punde.
Klabu ya Simba itaendelea kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za mpira wa miguu kama ambavyo imekuwa ikifanya.
Klabu ya Simba imeandika taarifa hiyo na kuichapa kwenye mitandao ya kijamii.
Simba itafunguliwa kufanya usajili wa wachezaji wapya wa ndani na wa kimataifa iwapo tu watakamilisha malipo ya deni hilo.
Klabu ya Simba inatarajiwa kufanya maingizo mapya mengi kwenye kikosi chake mapema kwenye dirisha dogo la usajili ambapo pia imepanga kuachana na nyota wake kadhaa wa kikosi cha kwanza.