Azam FC

MTIBWA VIBONDE KWA AZAM

Published on

Kwa takribani misimu mitatu mtawalia, Mtibwa Sugar wameendelea kuwa vibonde wa Azam Fc haijalishi wanacheza uwanja gani. Tangu msimu wa 2021, Mtibwa Sugar hajawahi kuambulia hata sare kwenye michezo 6 ya mwisho waliyocheza, yote akiangukia pua.

Mtibwa Sugar leo wanaingia kwenye uwanja wa Chamazi wakiwa na kumbukumbu mbaya  kwenye uwanja huo mara ya mwisho walipokutana wakikubali kichapo cha mabao 2-1. Kana kwamba haitoishi hawapo kwenye muendelezo mzuri wa kimatokeo na hata wakiwa uwanjani huoni wakicheza vizuri. Tangu washinde 3-1 dhidi ya Geita Gold kwenye uwanja wao wa Nyumbani, Manungu, wameenda kufungwa mechi 2 mfululizo(1-0 v KMC na 2-1 v JKT Tanzania) wakiwa chini ya kocha Zuberi Katwila.

Hivi Karibuni Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Ndg, Malima alipowatembelea kambini aliwapa changamoto ya kuhakikisha wanarejea kwenye makali yao na kuanza kupata matokeo hata kama hawatocheza soka la kuvutia, akichagiza zaidi kuwa wakusanye walahu alama 12 kati ya 18 ya michezo 6 ijayo wakianza na mchezo waleo dhidi ya Matajiri wa Chamazi.

Azam kwa upande wao hawana presha sana, wapo nafasi ya 2 wakiwa na alama zao 19 lakini wanaamini kuwa safari ni ndefu na kila pointi ni muhimu kwenye ligi msimu huu. Wenyewe wametoka kushinda michezo yao miwili mfululizo ya ligi kuu lakini na mchezo mmoja wa kirafiki. Wakishinda 3-0 ugenini dhidi ya Mashujaa kabla ya kushinda 3-1 ugenini tena dhidi ya Ihefu na mchezo wa kirafiki wakiwafunga JKU 3-1 kwenye uwanja wa Chamazi.

Alama 3 zina umuhimu sana kwa timu zote mbili leo. Nani atazitwaa? Majibu tutayapata kuanzia mishale ya 12.30 jioni ya leo wanaume hawa watakapomenyana kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi.

Popular Posts

Exit mobile version