Klabu ya Sinba ya Jijini Dar Es Salaam leo imebanwa mbavu na kutoka sare ya kufungana goli 1-1 dhidi ya Asec Mimosas ya nchini Ivory Coast katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Barani Afrika uliofanyika katika dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar Es Salaam.
Goli la Simba lilifungwa kipindi cha kwanza na Saidi Ntibanzokiza kwa mkwaju wa penalty baada ya mchezaji mmoja wa Asec Mimosas kuunawa mpira uliopigwa na Kibu Denis ndani ya eneo la 18.
Goli la kusawazisha la Asec mimosasa likifungwa mapema kipindi cha pili na nyota Pokou akimalizia kazi safi iliyofanywa na Karamoko aliyetokea benchi.
Baada ya mchezo huo mashabiki na wanachama wa kikosi cha Simba walitamalaki nje ya uwanja wa Taifa wakiisubiri timu yao itoke ili pengine waelezee hisia zao kwa viongozi na mashabiki wa timu hiyo, huku kila mmoja akitoa maoni yake.
Wachezaji hawajitumi.
Shabiki mmoja wa Simba alisema.
Nafasi bado ipo tukiwafunga Jwaneng kwao na hapa kwetu na tukatoa sare na Wydad kwao na hapa kwetu tukashinda tunafuzu.
Shabiki mwingine wa Simba alieleza.
Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo Ismail Aden Rage ameeleza chanzo cha Simba kutokufanya vizuri ni kutokana na wachezaji kutokujituma wanapokuwa uwanjani.
Wachezaji wa Simba hawana nguvu, hawana stamina, hatuelewi wanacheza formation gani, kwa mpira huu hatuwezi kwenda popote, lazima wafanye marekebisho.
Ismail Rage, Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba.
Afisa Habari wa klabu ya simba Ahmed ameeleza sababu ya mashabiki kuwa na mwitikio mdogo wa kufika uwanjani kuwa ni pamoja na matokeo yasiyoridhisha yanayopatikana kutoka kwa timu yao lakini kwasasa wanaelekeza macho yao kwenye michezo inayofuata.
Tumepoteza alama mbili, bado alama zingine nyingi zinatusubiri mbele, yaani liwalo na liwe.
Mashabiki hawaji uwanjani kwasababu hatupati matokeo mazuri, tumeshajiwekea mazingira kwamba lazima tushinde mchezo huu.
Presha inaongezeka, kazi inaongezeka ni lazima sasa tukashinde Botswana ili tufufue matumaini.
Ahmed Ally, Afisa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba.
December 2, 2023 saa 10:00 Jioni, Simba itakuwa na mchezo wa pili wa hatua ya makundi dhidi ya Jwaneng Galaxy nchini Botswana siku chache zijazo.