NBC Premier League

TANZANIA PRISONS WAING’ANG’ANIA IHEFU MBARALI

Published on

Ihefu na Tanzania Prisons wametoshana nguvu kwa kutoka suluhu ya 0-0 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara mchezo uliopigwa kwenye dimba la Highland Estates na timu zote kuondoka na alama 1.

Kipute hiki cha kukata na shoka kilianza na dakika 45 za moto sana huku wenyeji Ihefu wakichukua mchezo kwa kiasi kikubwa. Kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo Ihefu walionyesha dhamira ya kutaka ushindi huku kocha Moses Basena akianza na mfumo wa 4-3-3 akitumia washambuliaji watatu, Mubarack Amza, Ismail Mgunda na Jaffary Kibaya, Lakini palikuwa na utulivu mkubwa kwenye safu ya ulinzi ya Prisons ikiongozwa na Jumanne Elfadhil.

Pengine ni miongoni mwa dakika 45 bora za Ihefu kwa mechi 3 za hivi karibuni. Ililazimu pia Yona Amos kufanya kazi kadhaa ziada ikiwemo kuupalaza mpira wa kichwa uliopigwa na Jaffary Kibaya huku Never Tigere aliyepiga vizuri mpira wake wa adhabu ulipaa kidogo juu ya lango.

Umiliki wa asilimia 51 kipindi cha kwanza dhidi ya 49 za Prisons huku wakipiga shuti 1 lililolenga lango, Ihefu walistahili kuwa mbele kipindi hiki cha kwanza pengine lakini walienda mapumziko 0-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kuingia bila mabadiliko yoyote. Huku Ihefu wakiendelezea walipoishia Kipindi cha kwanza japokuwa bado palikosekana utulivu. Dakika ya 53 Ismail Mgunda alikuwa karibu kuipatia timu yake goli lakini kichwa alichopiga kilikuwa chepesi kwa mlinda lango Yona Amos. Dakika hizi Joseph Mahundi na Charles Ilanfya walitambulishwa mchezoni kuchukua nafasi za Never Tigere na Jaffary Kibaya upande wa Ihefu. Huku Joshua Nyantini akichukua nafasi ya Omary Abdallah upande wa Prisons.

Mpira ulionekana kupooza dakika kadhaa za kipindi cha pili huku Prison wakionyesha utulivu. Ihefu waliaamua kufanya mabadiliko kwa kuwaingiza Viberenge Nassor Saadun na Rashid Juma na kuwatoa Mubarack Amza na Ismail Mgunda walioonekana kupungua maarifa. Kila timu ilikuwa inakosa maarifa hasa kwenye eneo la mwisho.

Dakika ya 71, Edwin Balua alidhania kaipatia timu yake ya Prisons mkwaju penati baada ya kufanyiwa madhambi na golikipa Fikirini Bakari wakati akilielekea lango lakini Muamuzi wa mchezo huu alikuwa na mawazo tofauti.

Dakika ya 81 Edwin Balua alishuhudia mpira wake adhabu kubwa ukienda kugonga nguzo ya pembeni na muda huo Raphael Daud Loth aliingia upande wa Ihefu huku Lambert Sabiyanka akichukua nafasi ya Jeremiah Juma upande wa Prisons wakiimarisha eneo la Kiungo.

Dakika ya 86 Samson Mbangula alikosa nafasi ya wazi baada ya kufanya jitihada kubwa lakini akiwa anammtizama Fikirini, mpira wake ulipaa juu ya Lango. Nafasi adhimu sana wanakosa Prisons.

Dakika zote 90 zinamalizika kwa suluhu ya 0-0. Matokeo haya yana maana kuwa timu zote zinabaki kwenye nafasi zao za sasa.

Popular Posts

Exit mobile version