CAF Champions League

YANGA KUMKOSA LOMALISA DHIDI YA MEDEAMA.

Published on

Klabu ya Young Africans inaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wake wa Ligi ya mabingwa Barani Afrika dhidi ya Medeama katika Jiji la Kumasi nchini Ghana.

Baada ya kuwasili na kuanza mazoezi katika mji huo, Afisa habari na mawasiliano wa klabu ya Yanga Ali Shaban Kamwe amesema kikosi kimewasili salama katika mji wa Kumasi na kinaendelea na mazoezi.

Kikosi kilianza safari Tanzania hadi Ethiopia ambapo kilipumzika kidogo na kisha kuunganisha hadi katika mji namba moja hapa Ghana wa Accra.

Baada ya kufika Accra kikosi kilipumzika kidogo na kisha kikaanza safari ya kuja katika mji namba mbili kwa ukubwa wa Kumasi ambapo ndipo mchezo wetu unachezwa siku ya Ijumaa.

Kikosi kimefanya mazoezi ya kwanza katika uwanja wa shule.

Ali Kamwe, Afisa habari na mawasiliano wa Young Africans.

Kwa upande wa meneja wa klabu ya Yanga Walter Harrison ameushukuru uongozi wa klabu hiyo kwa kuwawezesha kufika mapema katika mji huo ili kuizoea hali ya hewa ya mji ambao mchezo wao utaenda kuchezwa.

Kwa kile ambacho tumekiona Kumasi, tunaamini tutakuwa kwenye wakati mzuri sana wa kujiandaa kuelekea kwenye mchezo huo.

Shukrani kwa uongozi kuweza kuhakikisha kwamba tunafika hapa mapema na kupata muda wa kutosha kujiandaa na kuijua hali ya hewa ya hapa Kumasi kabla ya kuingia kwenye mchezo.

Walter Harrison, Meneja wa klabu ya Young Africans.

Daktari wa timu, Moses Etutu ametoa maelezo juu ya hali ya wachezaji ilivyo kwasasa pamoja na majeruhi watakaokosekana katika mchezo wao dhidi ya Medeama.

Tunategemea Lomalisa ndani ya wiki moja atakuwa yupo sawa na atarejea kwenye uwanja wa mazoezi kwani majeraha yake sio makubwa sana.

Wachezaji wote waliofika hapa Kumasi wapo salama, hatuna majeruhi kwenye kikosini na hatuna magonjwa ambayo yanaweza kumzuia mchezaji kucheza kwenye mechi labda kocha aamue.

Moses Etutu, Daktari wa timu ya Young Africans.

Young Africans itakuwa kibaruani Ijumaa hii ikisaka alama tatu [3] za kwanza katika michuano ya kimataifa kwenye Ligi ya mabingwa Barani Afrika.

Yanga inashika mkia katika kundi lake ikiwa imecheza michezo miwili na imevuna alama moja pekee huku Medeama ikicheza michezo miwili [2] na imevuna alama tatu [3].

Yanga imefungwa na CR Beluizdad [A] na imetoa sare na Al Ahly [H].

Medeama ilipoteza mbele ya Al Ahly [A] na ikashinda mbele ya CR Belouizdad [H].

Popular Posts

Exit mobile version