Klabu za Azam FC na KMC ziko moto na leo usiku zinakutana kwa mara ya kwanza msimu huu katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC. Timu hizo zinakutana kuanzia saa 3 usiku, baada ya Bodi ya Ligi kuurudisha nyuma mchezo huo ambao awali ratiba ilionyesha ungechezwa kesho Ijumaa, huku kila moja ikiwa na kiu ya kusaka pointi tatu ili kuziweka pazuri kwenye msimamo.
Azam ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 22 baada ya mechi 10, ikifunga mabao 24 na kufungwa tisa, huku KMC ikishika nafasi ya tano ikiwa na pointi 19, ikifunga mabao 13 na kufungwa mabao 14.
Kama Azam itashinda mchezo huo itapaa hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiing’oa Yanga SC yenye alama 24 kwa sasa, kwani Wana lambalamba hao watafikisha 25, lakini ikilazimishwa sare inaweza kuongeza pengo la pointi kati yao na Simba ilipo nafasi ya tatu na pointi 19 kama ilizonazo KMC. Kwa namna timu hizo zilivyo na ushindani uliopo ni wazi haitakuwa mechi nyepesi.