Wenyeji Medeama walikuwa mbele kiuchezaji walionyesha dhamira ya kutaka alama 3 nyumbani kwa dakika za mwanzo za mchezo huku kurejea kwa Jonathan Sowah kwenye safu ya ushambuliaji kukileta uhai na uhatari zaidi kwenye mfumo wao wa 4-3-3.
Medeama walitangulia kupitia kwa mkwaju wa penati dakika ya 27 baada ya winga Derrick Fordjour kuchezewa madhambi kwenye eneo la penati na Dickson Job. Jonathan Sowah alipiga penati hiyo kiufundi na kuitanguliza timu yake.
Licha ya Yanga kuonekana kuwa chini kimchezo huku leo wakitumia mfumo wa 5-3-2 lakini Pacome Zouzoua alionekana binafsi kuwa hai na kusukuma mashambulizi mbele. Maxi hakuonekana kuwa na hatari sana dakika hizi huku pakionekana hakuna mipira ya hatari iliyowafikia Clement Mzize na Kennedy Musonda.
Dakika ya 36, Pacome Zouzoua alitumia uzembe wa Derrick Fordjour na kumpokonya mpira kisha kukimbia nao kabla hajaachia shuti kali la chini chini lililomuacha golikipa Felix Kyei asiwe na cha kufanya mpira ukitinga nyavuni kuisawazishia timu yake ya Yanga.
Mpaka mapumziko Medeama 1-1 Yanga.
Kipindi cha pili kilikuwa wazi zaidi kwa timu zote mbili kushambuliana na kusaka alama 3. Kila timu ikitengeneza nafasi lakini ulikosekana umakini wa kumalizia.
Mwalimu Gamondi aliamua kumuingiza Azizi Ki akichukua nafasi ya Clement Mzize yakiwa ni mabadiliko ya kiufundi ili kuongeza ufanisi na kasi zaidi kwenye safu ya ushambuliaji ila bado hakutoka kwenye mfumo wake.
Medeama pia walifanya mabadiliko kadhaa hasa kwenye safu yao ya ushambuliaji lakini bado hapakuwa na ufanisi kwenye umaliziaji.
Mchezo uliendelea kuwa wazi kwa yoyote kupata matokeo lakini ni kama uliandikiwa kuisha sare. Licha ya mashambulizi ya kujibizana mfululizo bado mchezo ulimalizika 1-1 huko kipindi cha pili kikimalizika bila goli.
Matokeo haya yamelifanya kundi kuzidi kuwa gumu huku ikizingatiwa pia matokeo ya Al Ahly na Belouizdad kuisha Suluhu. Bado timu zote 4 zina nafasi ya kufuzu na michezo mitatu ya mwisho inatarajiwa kuwa migumu sana kwa timu zote Yanga, Al Ahly, Belouizdad na Medeama.