NBC Premier League

SIMBA “NUSU PEPONI, NUSU KUZIMU”

Published on

Klabu ya soka ya Simba leo imekosa nafasi ya kupunguza tofauti ya alama na walio juu yake kwenye msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na KMC kwenye mchezo uliopigwa kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi.

Wenyeji wa mchezo huo, KMC walitangulia kupata bao la utangulizi dakika ya 30 ya mchezo kupitia Waziri Junior Shentembo akimalizia vizuri kazi yake mwenyewe baada ya kuwazidi mbio na maarifa walinzi wa Simba.

Simba walionekana kucheza chini sana ya uwezo wao huku wakikosa utulivu hasa kwenye eneo la kumalizia hivyo kuwaruhusu KMC kujiamini ya kuwa wanaweza kupata matokeo mbele yao.

Hapakuwa na ubunifu wa kutosha hasa kutoka kwa viungo washambuliaji, Saido, Onana na Kibu huku malisho machache kwa John Bocco nayoa hayakuwa yenye kuzaa matunda.

KMC Walienda Mapumziko wakiwa kifua mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Simba walirejea na mabadiliko hasa eneo la ushambuliaji na wakionekana kuwa na kiu ya kusaka magoli tofauti na kipindi cha kwanza.

Saido Ntibazonkiza aliisawazishia Simba dakika ya 57 ya mchezo kwa mkwaju wa penati na kuifanya Simba kufufua matumaini ya pengine kuibuka na alama zote tatu(3).

Dakika ya 62 tu, akitokea benchi, Jean Othos Baleke aliiandikia Simba bao la 2 na kuwapa uongozi kwa mara ya kwanza kwenye mchezo huu uliosheheni ushindani wa aina yake.

Simba walionekana kurejea kwenye usukani wa mchezo lakini bado waliendelea kushindwa kutumia nafasi walizokuwa wakizitengeneza. Ubaya ni kwamba waliruhus KMC waone bado lolote linawezekana.

Wakati watu wakiamini alama 3 zinakwenda Msimbazi, Waziri Junior alikuwa hajamalizana na Ayoub Lakred. Shuti kuli lililopigwa na Tepsie Evans, dakika za lala salama kabisa lilimpalia golikipa Ayoub Lakred na mpira kumdondokea vizuri Mfungaji ambaye bila ajizi aliachia kiki kali lililomshinda golikipa Lakred. Wanasimba hawakuamini walichokiona.

Dakika zote 90 za mchezo zinatamatika, KMC 2-2 Simba. Matokeo haya yanaibakisha Simba nafasi ya 3 wakiwa na alama zao 23, alama 4 nyuma ya Yanga walio nafasi ya 2 na alama 27 na alama 8 nyuma ya vinara Azam wenye alama 31.

Popular Posts

Exit mobile version