Kocha mpya wa Dodoma Jiji, Baraza amesema kuwa Kuja kwake Dodoma ni kwasababu kaaminiwa anafaa kwa ajili ya timu hiyo na hasa maendeleo ya muda mrefu na ya muda mfupi kwakuwa pia huwa haitaji sana muda kuweka mipango yake yote sawa hasa linapokuja suala la wachezaji.
Huwa situmii muda mwingi kuangalia mchezaji kama ananifaa au la. Hata kama mchezaji akija kwenye majaribio kwenye timu yangu ni siku 1 tu inanitosha, kuangalia miguso yake ya mpira, mikimbio hata kama hayuko fiti. Wapo wengine wataangalia ufiti wake kwenye timu yangu ila mimi sihitaji wiki nzima kujua uwezo wa mchezaji na kama atanisaidia au hatonisaidia ili tusipotezeane muda.
Kocha Baraza pia hakusita kusema anamfahamu kwa kiasi gani Denis Nkane na uwezo wake na utayari wa kufanya naye kazi.
Kiukweli Denis nlimmtazama mazoezini nakumbuka ilikuwa tunaend kwenye mechi dhidi ya Simba. Nikamwambia nakupa nafasi kesho. Na kweli alicheza vizuri na alimzima kabisa yule mchezaji wa Simba(Chikwende) walimsajili dirisha dogo. Mengine nadhani yako chini ya uongozi lakini kwa mimi hata yeye anajua ni kiasi gani namuhusudu na napenda kufanya naye kazi
Aliongeza pia kuhusu safari ya Novatus Dismas Miroshi.
Novatus Dismas huyu mnaemuona leo mimi ndio nlipendekeza asiachwe maana nilimkuta ofisini kwa Katibu anamalizana na timu aondoke lakini mimi nikasema naomba nimuone mazoezini. Kesho yake tu nlimuambia aje mazoezini na alivyokuja kunionesha mazoezini nikapendekeza abaki na huo msimu akaja kuwa Mchezaji Bora Chipukizi nadhani na mengine ni Historia. Na wapo wengi tu akina David Mgore, Deogratius Mafiye. Hawa ni wale ambao nilikuwa nao Biashara United tu. Ukiachana na akina Kapama niliowakuta Kagera.
Vipi kuhusu kuchukua timu kwenye nyakati hizi?
Mimi napenda changamoto sana sisemi kuwa sipendi mteremko yani kupata timu ambayo ipo nafasi nzuri, lakini nafurahia Changamoto na kupambana na hizi timu ambazo labda zinakuwa kwenye nafasi mbaya au zinahitaji kurejesha makali yake na kurudi kwenye malengo yake. Na nashukuru nafanikishaga kwa kiwango kikubwa tu. Timu zote hizi, Biashara, Kagera nimezikuta kwa mazingira hayo na kuziacha Salama.
Kwanini Dodoma Jiji?
Kwanza nimsifu huyu Katibu wa Dodoma, amekuwa akinifuatilia sana na kunisumbua kweli tangu nikiwa Kagera. Kwahivyo haikuwa kazi ngumu kunishawishi safari hii hasa ukizingatia nilikuwa nshamalizana na timu Kenya. Nikahisi ni wakati sahihi kwenda kuwatumikia watu wa Dodoma na kiukweli naona kabisa ntapata ushirikiano mkubwa hapa kutokana na imani yao kwangu
Kupata wachezaji wapya dirishi hili dogo ili kuongezea nguvu kikosi chake, Baraza alikuwa na hili la kusema juu ya mipango yake.
Kwa sasa nahitaji wachezaji walio tayari na sio wa kuja kukaa benchi. Bila shaka kuna hii michuano inaanza sasa ya Mapinduzi imekuwa ni sehemu nzuri pia ya kupata wachezaji wazuri tu wenye uwezo mkubwa. Sehemu moja wapo ntayoitumia kupendekezea wachezaji ni hapo pia ili nipate wachezaji wa kuja kuipambania timu
Francis Baraza pia alimalizia na kusema kuwa mpango ni kuifikisha Dodoma Jiji mbali zaidi hapo baadae ila kwa msimu huu ni kupambana walahu kuendelea kubaki kwenye nafasi 7, 5 mpaka 4 za juu na uwezo huo wanao kwakuwa wana wachezaji wazuri.
Dodoma Jiji walishinda mchezo wao dhidi ya Ihefu 1-0 wakati Baraza anatangazwa lakini hakuwa kwenye Benchi, timu ikisimamiwa na Kassim Liogope. Kwa sasa wanashikilia nafasi ya 7 kwenye msimamo wa NPL wakiwa na alama 18 baada ya michezo 13.