Michuano ya kombe la mapinduzi inatarajiwa kuendelea tena kesho hatua ya robo fainali baada ya hapo jana kutamatika kwa michezo ya hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Klabu ya Yanga kesho inatazamiwa kushuka dimbani majira ya saa 2:15 usiku katika uwanja wa New Amaan Complex kuikabili klabu ya APR kutoka Rwanda katika mchezo wa robo fainali ya kombe la mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.
Kuelekea katika mchezo huo kocha msaidizi wa klabu ya Yanga Mussa Ndaw amesema kesho wao ndio wanayaanza rasmi mashindano hayo na wanampango wa kuweka kikosi kizima kwenye mchezo huo.
“Kesho tuna mchezo mwingine, mchezo wa mtoano sio kama michezo iliyopita, kesho ndio tunaanza rasmi mashindano”.
“Uliona mchezo uliopita tulitumia wachezaji wengi wa U20, wachezaji wengi waliocheza mchezo wa mwisho watapumzika”.
“Kesho tutawatumia wachezaji wa kikosi cha kwanza japo wengine wapo kwenye fainali za mataifa ya Africa [AFCON], tupo hapa na kesho tutaenda kushinda Inshallah”.
“Tupo tayari kwaajili ya mchezo wa kesho na wachezaji wapo tayari, tupo tayari pia hadi mwisho wa mashindano”.
Kocha Mussa Ndaw pia alieleza hali ya nyota wake Augustine Okrah ambaye alipata majeraha kwenye mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya KVZ inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu hospitalini alipopelekwa baada ya kuvunjika mfupa wa pua.
“Okrah kwasasa yupo vizuri kwasababu tulimpeleka hospital kwa siku mbili kwaajili ya uchunguzi, lakini kwasasa yuko vizuri, amekuja hotelini”.
“Kitu cha msingi ni afya yake, tuna michezo mingi mashabiki watamuona, mashabiki watamuona, tukifika nusu fainali au fainali”.
Kwaniaba ya wachezaji kiungo mshambuliaji wa klabu ya Yanga Denis Nkane amesema wamejiandaa vyema kuelekea mchezo huo ili waweze kutimiza malengo ambayo wamejiwekea kwenye mashindano hayo.
“Tumejiandaa vizuri kuhakikisha mchezo kwa kesho tunafanya vizuri, ili kuhakikisha tunatimiza kile kilichotuleta huku”.
“APR ina wachezaji wenye uzoefu Afrika na inawachezaji wanaojua umuhimu wa mechi ya kesho, sisi kama wachezaji tunafahamu mechi ya kesho haitakuwa rahisi”.
“Sikupata muda wa mwingi wa kucheza kwenye Ligi lakini hii ni nafasi yangu kama mchezaji kumshawishi mwalimu”.
Yanga itashuka dimbani kesho majira ya saa 2:00 usiku kuikabiri APR ya Rwanda katika hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi ambayo inaendelea visiwani Zanzibar.
Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa imeshinda michezo miwili [2] na kutoa sare mchezo mmoja [1] ikifunga magoli saba [7].