AFCON

SAMATTA: SIO VITA YANGU NA SALAH NI VITA YA TAIFA.

Published on

Timu ya Taifa ya Tanzania hii leo itakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Misri ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea michezo ya fainali za AFCON 2023 nchini Ivory Coast.

Huu ni mchezo wa kwanza na wa mwisho wa maandalizi kwa kikosi cha wachezaji 27 cha mwisho watakaosafiri kuelekea nchini Ivory Coast wakitokea nchini Misri walipoweka kambi ya maandalizi.

Kuelekea mchezo huo wa leo utakaopigwa saa 19:00 Usiku nahodha wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Ally Samatta amesema maandalizi yanaenda vyema hadi hivi sasa.

“Maandalizi yanaenda vizuri, wachezaji wanafahamu umuhimu wa maandalizi na umuhimu wa mchezo wa kesho wa kirafiki dhidi ya Misri”.

“Misri ni wapinzani ambao ukiwaangalia kwa karibu wanaweza kuwa wanafanana na Morocco ambao tutacheza nao mechi ya kwanza kwenye michuano ya AFCON, utakuwa ni mwananga mzuri kwa walimu na wachezaji kujipima nguvu, kabla hatujaenda kucheza mechi yetu ya kwanza dhidi ya Morocco”.

Mara kadhaa pia nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Ally Samatta amekutana na Mohamed Salah, amewahi kukutana nae kwenye michuano ya UEFA na Ligi kuu nchini England lakini mara hii anasema hautakuwa mchezo wa Salah na Samatta bali utakuwa mchezo wa kuangalia mbinu za walimu nini waboreshe kabla ya kuanza michuano ya AFCON.

“Ukiangalia ni mchezo wa walimu kuangalia mbinu zao, sijafikiria kama ni mchezo wa Mohamed Salah na Mbwana Samatta, au wa Saimon Msuva na Treziguet, nadhani ni mchezo kati ya Taifa Stars dhidi ya Misri, wakijipima nguvu kuangalia ni kitu gani watarekebisha”.

” Ni mchezo mzuri kwa Misri lakini ni mchezo bora sana kwa Tanzania, ni mchezo ambao utawapa nafasi walimu kuangalia nini waongeze, katika maandalizi ya kuiandaa timu ya Taifa ya Tanzania”.

Timu ya Taifa ya Tanzania inashuka dimbani majira ya saa moja za usiku kuikabili timu ya Taifa ya Misri ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea fainali za mataifa ya Afrika [AFCON 2023] zinazotarajiwa kuanza kurindima January 13, 2024 nchini Ivory Coast.

Mara baada ya mchezo huu wa leo kikosi cha wacheza 27 cha timu ya Taifa ya Tanzania kitaianza safari rasmi siku ya kesho Jumatatu kuelekea nchini Ivory Coast na January 17 kitacheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Morocco.

Watanzania wanaitakia kila lakheri timu yao ya Taifa katika fainali za AFCON huku wakiwa na matumaini safari hii ya kufanya vizuri zaidi ya makala mbili za AFCON ambazo timu hiyo ilishiriki.

Popular Posts

Exit mobile version