Mechi kati ya Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu ya Soka la wanawake, JKT Queens dhidi ya Mabingwa mara nyingi zaidi wa ligi hiyo Simba Queens imeshindwa kuchezeka kutokana na sintofahamu iliyojitokeza uwanjani.
Timu ya Simba Queens iliwasili kwenye Uwanja wa Azam Complex kwa ajili ya kipute hicho kilichokuwa kinasubiriwa kwa hamu na wapenda soka wengi hasa kutokana na ushindani wa hivi karibuni wa timu hizo mbili, lakini timu ya JKT Queens haikutokea uwanjani mpaka kufikia 10.30 jioni.
Kwa mujibu wa JKT Queens, wao walikuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Major General Isamuhyo uliopo Mbweni kuwasubiri Simba Queens lakini wao ndio hawakutokea.
Taarifa za kina zaidi zinasema kuwa timu zote zilifika kwenye mkutano wa kabla ya mechi pamoja na waamuzi huku ikifahamika kabisa kuwa mchezo utapigwa kwenye dimba la Azam Complex, lakini katika hali iliyozua taharuki kiwanjani hapo ni Simba Queens pekee ndio waliofika kiwanjani hapo sambamba na maofisa wote wa mchezo husika wakiwemo waamuzi wote wa mchezo huo.
Kunako Uwanja wa Major General Isamuhyo hali ilikuwa tofauti, pakiwa na timu ya JKT Queens pekee pamoja na baadhi ya maofisa wa timu hiyo na mashabiki wachache waliojitokeza uwanjani hapo huku pakiwa hakuna ofisa hata mmoja wa mchezo huo.
Waamuzi waliwaamuru Wachezaji wa Simba Queens warejee vyumbani wakisubiri taratibu zingine na muongozo kutoka kwenye mamlaka za juu za soka kuhusu nini kitafuata kwenye taarifa rasmi baada ya kuhairisha mchezo huo.