Makala Nyingine

NYOTA KIBAO KUIKOSA AFCON

Published on

IFUATAYO NI ORODHA YA WACHEZAJI WAKUBWA/MUHIMU WATAKAOKOSEKANA KWENYE MASHINDANO YA AFCON 2023.

  1. Victor Boniface(Nigeria) anaongoza orodha ya wachezaji wakubwa na muhimu kwenye timu zao watakaokosekana kwenye michuano hii mikubwa barani Africa.
    Akiwa amelitumikia taifa lake mara 5 tu, mshambuliaji huyu wa Bayer Leverkusen, amekuwa kwenye kiwango bora mno tangu ajiunge na timu hiyo kutokea Union St. Gilloise ya Ubelgiji akifunga mabao 10 kwenye michezo 16 aliyocheza lakini bado hajafanikiwa kulifungia taifa lake hata bao moja, pengine ilikuwa nafasi yake kuhamishia makali yake ya Bundesliga kwenye timu ya taifa lakini atayakosa mashindano hayo kwasababu ya majeraha ya Nyonga.

2. Wilfried Ndidi(Nigeria)
Taarifa ya Enzo Maresca, kocha wa Leicester City ya kuwa kiungo wao Wilfried Ndidi atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu akiuguza majeraha ya misuli, pengine ni miongoni mwa taarifa mbaya sana kwa Super Eagles kuelekea AFCON.

Ndidi amekuwa ni muhimili mkubwa sana eneo la kiungo kwa Nigeria na kukosekana kwake kunampa wakati mgumu sana kocha wa Nigeria, Jose Peseiro.

  1. Taiwo Awoniyi(Nigeria)
    Mchezaji huyu amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu akiwa na timu yake ya NOTTINGHAM FOREST. Hapakuwa na shaka ya yeye kuliwakilisha taifa lake la Nigeria AFCON kwa mara ya pili lakini kocha wa klabu yake Steve Cooper alitangaza hivi karibuni kuwa Awoniyi atakuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili kwa tatizo la nyonga.
  1. Bryan Mbeumo(Cameroon)

Pigo kubwa sana hili kwa Simba wasiofugika kummkosa Mbeumo kwenye toleo hili la AFCON huku sasa wakibaki kumtazamia Zaidi Vicent Aboubakar kama Mshambuliaji kinara pekee licha ya uwepo wa Frank Zambo Anguissa na wengineo.

Mbeumo amekuwa bora sana kwenye timu yake ya Brentford akifunga mabao 7 kwenye mechi 15 alizocheza na pasi za usaidizi 4. Alipata majeraha kwenye mchezo dhidi waliopoteza dhidi ya Brighton, Disemba 6 na alitarajiwa kuwa nje kwa takribani wiki 12.

  1. Cheickhou Doucoure(Mali)

Akionekana kuondoshwa na machela kabla ya kuondoka uwanjani Kenilworth Road akiwa na “magongo” Kwenye mechi waliopoteza 2-1 dhidi ya Luton, Crystal Palace walithibitisha kupitia kocha Roy Hodgson kuwa atakuwa nje kwa muda mrefu sana, si chini ya miezi 6.

Doucoure sio tu atakosa mashindano ya AFCON na kuwa pengo kubwa kwa timu yake ya Mali lakini pia msimu wake wa soka wa 2023/24 umetamatikia hapo.

  1. Ibrahima Kone (Mali)

Wakati wakiendelea kuugumia maumivu ya kumkosa Doucoure, pengine hili ni pigo jingine kubwa sana kwa Mali.
Akiwa na miaka 23 tu, akiichezea Almeria ya Uhispania, rekodi zake kwenye timu ya taifa ni za kutisha sana kiasi cha kwamba kumkosa kwenye mashindano hayo ni pigo kubwa kwa taifa la Mali chini ya Kocha Eric Sekou Chelle.

Akiwa kafunga mabao 12 kwenye mechi 16 alizotumikia taifa lake, mshambuliaji huyu aliumia kifundo cha mguu kwenye mchezo dhidi ya Uganda na atakosa AFCON akiuguza jeraha.

  1. Joseph Aidoo(Ghana)

Kitasa hiki cha Celta Vigo akihudumu vema nafasi ya mlinzi wa kati kwa timu hiyo ya Uhispania, amekuwa ni muhimili mkubwa pia kwenye safu ya ulinzi ya Black Stars.

Akiumia kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Mexico mapema mwezi oktoba 2023, klabu yake ilithibitisha kuwa hatorejea uwanjani kabla ya miezi 6-7. Kitasa hiki kimemaliza msimu wake wa mashindano.

  1. Tariq Lamptey(Ghana)

Akisifika kwa kasi yake, winga huyu hatari wa Brighton mzaliwa wa Uingereza mwenye asili ya Ghana anakuwa pengo jingine kwa Ghana kwenye AFCON ya mwaka huu.

Lamptey alitoka uwanjani akichechemea kwenye mchezo waliopata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Nottingham forest na taarifa zaidi baadae zikasema kuwa atakosekana kwa muda wa miezi mitatu(3).

  1. Kamaldeen Sulemana(Ghana)

Pengine baada ya zaidi ya miaka 40 kupita tangu mara ya mwisho watwae ubingwa wa AFCON waliona huu ni mwaka wao wa kurejesha heshima yao Afrika, lakini Kamaldeen Sulemana anongeza idadi ya wachezaji muhimu wa kuwafikisha nchi ya ahadi.

Sulemana, 21, aliumia wakati anaitumikia timu yake ya SOUTHAMPTON na kocha Russel Martin alithibitisha kuwa hatoweza kurejea mapema kuiwahi AFCON kutokana na tatizo la misuli ya paja.
Awali alijumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 55 cha awali kilichoitwa na Kocha Chris Hughton kwa ajili ya AFCON lakini isivyo bahati, majeraha yamemtenganisha.

Popular Posts

Exit mobile version