Klabu ya AS Roma imetangaza kuachana na kocha wake raia wa Ureno Jose Mourinho aliyedumu kikosini hapo kwa takribani miaka mitatu.
AS Roma ilimtangaza Mourinho kuwa kocha wake mkuu mnamo May 2021 akiwa ni kocha wa 60 wa kuifundisha klabu hiyo.
Mourinho aliiongoza klabu hiyo kushinda ubingwa wa kwanza wa UEFA Conference League na kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa huo huko Tirana May 25, 2022.
Pia Mourinho aliifanikisha Roma kufika fainali ya Europa League iliyochezwa huko Budapest msimu uliopita.
AS Roma imemshukuru Jose Mourinho kwa mafanikio aliyoyapata akiwa na klabu hiyo.
“Tunapenda kumshukuru Jose, kwa niaba yetu sisi wote hapa AS Roma kwa nguvu yake ya upambanaji tangu alipofika hapa Roma”.
“Siku zote tutakuwa na kumbukumbu nzuri juu ya mafanikio yake hapa Roma, lakini tunaamini mabadiliko ya haraka ni kwaajili ya manufaa ya klabu”.
“Tunamtakia kila lakheri Jose na wasaidizi wake kwenye maisha yao mapya yajayo”.
Klabu hiyo pia imeweka wazi kuwa baada ya kuachana na Kocha Jose Mourinho sasa inaangalia utaratibu wa kumpata kocha mwingine atakayechukua mikoba ya Jose Mourinho.