Klabu ya Singida Fountain Gate kwa kipindi cha hivi karibuni imekutana na rungu la kufungiwa na shirikisho la soka Duniani FIFA na TFF kwa kushindwa kuwalipa nyota wake wa zamani waliowahi kuitumikia klabu hiyo.
Singida ipo kwenye kipindi cha ukata wa fedha kwani imeshindwa kabisa kulipa madeni hayo kitu ambacho kimepelekea kuwauza nyota wake kadhaa wa kikosi cha kwanza kwenda nje ya nchi na ndani ya Tanzania.
Rais wa klabu hiyo Japhet Makau ameweka wazi kuwa Siñgida Fountain Gate imemuuza mlinzi wake Gadiel Michael kwenda nchini Ivory Coast ili ipate pesa ya kulipa madeni yanayoikabili.
“Katika siku za hivi karibuni, klabu yetu imekuwa ikipata majanga mengi, kufuatia kufungiwa na FIFA na TFF kutokana na madai kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea kutokana na wachezaji wetu”.
“Kwasehemu kubwa, inaweza kuwa inachangiwa na jinsi ambavyo tunaingia mikataba siku za nyuma, na jinsi ambavyo tunapaswa kuachana na wachezaji wetu”.
“Klabu ya mpira haiwezi kuendeshwa bila kusajili wachezaji, kuna nyakati lazima utasajili wachezaji, ili kufika mahali lazima tumalizane na wachezaji wetu ili kuweza kufunguliwa na FIFA na klabu tuweze kusajili”.
“Ili kutatua changamoto zilizopo lazima tuzungumze na wachezaji na watu wote ambao tunadaiana, na kuhakikisha kwamba tunaweka mambo yetu vizuri”.
“Kitu cha pili, kuona jinsi ambavyo tunaweza kutafuta fedha kuhakikisha kwamba tunalipa yale madeni yote”.
“Kama klabu shughuli yetu kubwa ni biashara ya mpira, na biashara hiyo inatokana na wachezaji, kwahiyo tukaamua kama klabu kuwaweka sokoni baadhi ya wachezaji wetu ambao tunadhani wanaweza kuwa na soko kubwa, na kuweza kutupatia pesa ambazo zinaweza kutusaidia kwenye changamoto ambayo tuko nayo”.
“Klabu kadhaa tumekuwa na mazungumzo nazo, ni kweli tumetoa wachezaji kadhaa kwenda kwenye klabu mbalimbali, wengine ndani ya nchi na wengine wakienda nje ya nchi”.
“Jambo la pili ni kupunguza matumizi na kubana gharama za uendeshaji, ili kuwa na klabu inayoweza kujiendesha vizuri bila madeni”.
“Tumewaachia baadhi ya wachezaji, mchezaji ambaye unamuondoa ni yule ambaye ana soko, lakini kwa wakati huo huo hauiathiri timu”.
“Gadiel Michael anaondoka leo kwenda Afrika kusini, kujiunga na klabu ya Cape town”.
“Ihefu ndio klabu iliyotimiza matakwa baada ya kuhitaji wachezaji wetu tukawapa wachezaji wanne au watano”, Japhet Makau, Rais wa Singida Fountain Gate.
Singida Fountain Gate licha ya kuondokewa na nyota wake hao lakini pia imempoteza Afisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo aliyetimkia kwenye klabu ya Ihefu inayoshiriki Ligi kuu Tanzania Bara.