Nyota wa kimataifa wa Ureno anayeitumikia klabu ya Al Nassr, Cristiano Ronaldo ameweka wazi kuwa tuzo za Ballon D’Or na zile za FIFA The Best zimepoteza mvuto.
Ronaldo ameweka wazi kuwa kwenye tuzo zozote zinazotakiwa kutolewa namba ndio kila kitu, kama zingetolewa kwa haki basi alistahili kubeba tuzo hizo.
Kwa upande mwingine pia Ronaldo ameweka wazi kuwa hajasema hayo kwasababu Messi alibeba tuzo bali vigezo walivyotumia kutoa tuzo hizo havikuwa sawa.
“Ballon D’Or na The Best zinapoteza uaminifu, namba ndio uhalisia”.
“Tunapaswa kuangalia msimu mzima, sio kwamba nasema Messi hakustahili hizo tuzo au Haaland au Mbappe, kifupi siziamini hizi tuzo”.
“Sio kwamba kwasababu nimeshinda Globe Soccer lakini huu ndio ukweli, namba zipo na hazidanganyi”.
“Hawawezi kuiondoa hii tuzo kwangu kwasababu ndio uhalisia, nina furaha kwasababu namba ndio ukweli”.
“Ukirejea nyuma kutazama kilichotokea Manchester United na Ureno, watu kiuhalisia wanafikiria nimeshindwa”.
“Lakini ukweli ni kwamba, niliweka umakini na nimekuwa na kipindi bora Al Nassr, ndio maana nimefunga magoli 54”, Alisema Ronaldo.
Cristiano Ronaldo licha ya kufunga magoli mengi mwaka jana lakini bado hakuwa sehemu ya nyota watatu bora waliotokea kwenye tuzo za Ballon D’Or zinazotolewa na shirikisho la soka nchini Ufaransa na zile za The Best zinazotolewa na shirikisho la soka Duniani (FIFA).