Timu ya Taifa ya Tanzania imeweka historia kwenye michuano ya AFCON 2023 tangu imeanza kushiriki kwa mara ya kwanza imevuna alama mbili.
Tanzania rasmi imeondoshwa kwenye fainali za AFCON 2023 baada ya kutoka sare kwenye mchezo wake wa mwisho dhidi ya Congo DR wa hatua ya makundi.
Kocha msaidizi wa Taifa Stars Juma Mgunda amesema kuwa kwasasa wataenda kuzungumza na shirikisho la soka nchini ili kurekebisha kikosi chao kwaajili ya michuano ijayo.
“Kwa uzito wa mashindano haya ulivyo, tutaenda kuzungumza na uongozi wa shirikisho kile ambacho tumekiona na uzoefu ambao tumeupata jinsi gani ya kujiandaa vizuri ili kuona mashindano yajayo tunafanya vizuri zaidi”.
“Kama mkijiandaa vizuri na mkiwa tayari lolote linawezekana, mataifa makubwa yalipokutana na madogo umeona walichokifanya, inaonekana tukijiandaa vizuri, tukijua umuhimu wa mashindano haya naamini kabisa na sisi ipo siku tutafanya maajabu”, Juma Mgunda, Kocha msaidizi Taifa Stars.
Tanzania ilipata pigo la kufungiwa kwa kocha wake mkuu Adel Amrouche baada ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya Morocco hivyo kikosi hicho kikawa chini ya kaimu kocha mkuu Hemed Suleiman Morocco.