Timu ya Taifa ya Angola imefanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali ya michuano ya AFCON 2023 baada ya kuinyuka timu ya Taifa ya Namibia kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa 1 wa raundi ya 16 Bora ya michuano hiyo huku ikisubiri Kumenyana na Nigeria kwenye hatua hiyo.
Mechi hiyo iliyoshuhudia timu zote zikimaliza na wachezaji 10 baada ya wachezaji wawili, mmoja wa kila timu kuonyeshwa Kadi nyekundu kwa matukio tofauti bado haikuacha kutoa burudani ya soka iliyotarajiwa kutoka kwa timu hizo mbili zote za ukanda wa COSAFA.
Golikipa wa Angola anayekipiga kwenye klabu ya Premiero De Agosto ya Angola, Neblu alikuwa wa kwanza kuonyeshwa kadi Nyekundu moja kwa moja dakika ya 17 tu ya mchezo baada ya kuzuia shambulizi kwa kudaka mpira nje ya eneo lake wakati mshambuliaji wa Namibia Bethuel Muzeu akijaribu kumnyanyulia ili afunge.
Beki wa Kati wa timu ya Namibia Lubeni Haukongo naye alionyeshwa kadi Nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya Njano ya pili kwa kosa la kumkwatua nyota wa Petro Atletico, Gilberto wakati akilielekea lango lao dakika ya 40 ya mchezo na kufanya timu zote kubaki na wachezaji 10.
Pancras Negras walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Nyota wao Gelson Dala akimalizia vema kazi nzuri ya kugongeana kati ya Gilberto na Fredy kabla hajakutana na pasi mtelezo kutoka kwa Alfredo Fredy na yeye kumalizia kiurahisi tu dakika 38 ya mchezo.
Namibia wakionekana kupoteana hasa nafasi ya ushambuliaji baada ya kutoka nje kwa kinda wao Prins Tijueza aliyepata majeraha ya kifundo cha mguu, Peter Shalulile akiwa chini ya kiwango chake leo na kumkosa mlinzi wao Haukongo wakajikuta wako nyuma kwa mabao mawili dakika ya 42 baada ya Gelson Dala tena kumalizia kwa kichwa mpira wa faulo uliochongwa vizuri na Alfredo Fredy.
Agostinho Mabululu alikuja kufunga Karamu ya magoli dhidi ya The Brave Warriors baada ya kufunga bao la 3 la kideo akiuzungusha mpira kwenye mwamba wa mbali kabisa na kumshinda Mlinda lango Lloyd Kazapua ambaye alikuwa na kibarua kigumu leo dhidi ya Majirani zao. Dakika ya 90, Angola 3-0 Namibia.
Kwingineko kwenye Dimba la Felix Houphouet- Boigny, Nigeria waliwasulubu Cameroon kwa kuwachapa mabao 2-0.
Ademola Lookman ndiye aliyepeleka kilio cha Wakameruni akipachika mabao yote mawili, moja kipindi cha kwanza na lingine kipindi cha pili.
Mchezo licha ya kutokuwa na kasi kama ilivyotarajiwa ulitawaliwa sana na mbinu na matumizi makubwa ya nguvu hasa eneo la katikati ya kiwanja. Eneo ambalo lilisababisha pasiwe na ufundi mwingi kwenye mechi hii wala pasi za maana za ushambuliaji bali ulihitajo juhudi binafsi.
Super Eagles walidhani wamepata bao la kuongoza dakika ya 9 tu ya mchezo kupitia kwa Mlinzi Semi Ajayi lakini lilikataliwa kwasababu ya mchezaji huyo kufaidika kuwa katika nafasi ya kuotea.
Dakika ya 36 Nigeria walipata bao la kutangulia likiwekwa kimiani na Ademola Lookman baada ya kazi kubwa binafsi iliyofanywa na Victor Osimhen kupora mpira mbele ya mlinzi wa Cameroon, Oumar Gonzalez kisha kumpenyezea pasi sukari mfungaji kuandika bao.
Cameroon wakiwa mbali kabisa na ubora wao hii leo walikuwa na nafasi finyu za kusawazisha bao hilo licha ya kuwa na washambuliaji kama Georges Kevin N’koudou, Frank Magri, Karl Toko Ekambi na hata alivyoingia Vincent Aboubakar bado hapakuwa na ubunifu hasa eneo la kiungo kutengeneza nafasi za wazi.
Lookman alishindilia goli lake la pili na msumari wa 2 kwa timu yake ya Nigeria kuhakikisha kuwa wanatinga hatua ya Robo Fainali akitumia tena madhaifu ya kupooza kwa safu ya ulinzi ya Cameroon kugongeana vema na Calvin Bassey kisha kupiga shuti lililomshinda golikipa wa Cameroon, Fabrice Ondoa. Dakika ya 90, Nigeria 2-0 Cameroon.
Nigeria wanafanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali hatua ambayo hawakuifikia msimu waa 2021 huku Angola wakifanya hivyo tangu walivyofanikiwa mwaka 2010 wakiwa waandaaji wa mashindano haya.