Klabu ya Kagera Sugar inatarajiwa kushuka dimbani kesho Ijumaa dhidi ya Yanga kwenye mwendelezo wa Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.
Kagera Sugar kupitia kwa Afisa habari na mawasiliano wa klabu hiyo Hamis Masanzala amewapa tahadhari mashabiki wa Yanga kuwa wasiende na matokeo kwenye mchezo wa kesho kwani utakuwa mchezo wa ushindani wa hali ya juu.
“Tumejiandaa kwaajili ya kushindana na kama tukipoteza basi ni Mungu tu atakuwa amependa, kikosi kimeandaliwa kwaajili ya kupambana”.
“Najua mashabiki wa Yanga wamesafiri kutoka mbali, mechi ya kesho ni mechi ya ushindani wasije na matokeo yao, tumejiandaa kwaajili ya kushinda”, Alisema Hussein Masanzala, Afisa Habari wa klabu ya Kagera Sugar.
Kuelekea katika mchezo huo pia Afisa habari wa Kagera Sugar ameweka wazi kuwa uongozi wa klabu hiyo umekuwa ukitoa “Bonus” kwa wachezaji wao pindi wanapoibuka na ushindi kwenye mechi zote lakini kwenye mechi dhidi ya timu kubwa “Bonus” inakuwa kubwa.
“Sisi huwa tunaweka Bonus kwa kila mchezo, tuna Bonus ya ushindi na Bonus ya kutoa sare, najua mechi ya kesho ni kubwa, wakishinda Bonus inakuwa kubwa zaidi”.
“Kwasababu ni mechi kubwa basi Bonus itakuwa kubwa, wasije wakasema tumewakamia, tutacheza kwa kadri ya uwezo wetu na maandalizi yetu yalipoishia”.
“Bonus inaweza ikazidi Million 10 kutokana na idadi ya wachezaji ambao tuko nao kwasababu inaanzia kwa wachezaji na benchi la ufundi”.
“Million 10 ni kiwango tu cha mchezaji mmoja mmoja, sio kwa pamoja kuna wale ambao watahusika kwenye mchezo na wale ambao watakuwa benchi lakini wanakuwa na Bonus zao iwapo tutapata matokeo hayo mawili [sare au ushindi]”, Hamis Masanzala.
Mchezo wa Kagera Sugar na Yanga unatarajiwa kupigwa Ijumaa ya kesho majira ya saa 10:00 Jioni katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, tayari Yanga imewasili mkoani Kagera kwaajili ya mchezo huo.