Klabu ya Simba imepewa kibali cha kuutumia uwanja wa New Amaan Complex uliopo visiwani Zanzibar kwaajili ya michezo yake ya Ligi iliyosalia baada ya uwanja wa Taifa kufungwa kupisha marekebisho.
Simba itaanza kuutumia uwanja huo February 18 kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, hivyo Simba itautumia uwanja huo katika michezo ya Ligi na Ligi ya mabingwa Barani Afrika.
Hata hivyo Simba itautumia uwanja wa CCM Kirumba kama uwanja wao wa nyumbani kwenye mchezo dhidi ya Azam FC, utakaopigwa Februari 9, baada ya hapo Februari 12 itacheza dhidi ya Geita Gold katika uwanja huo huo wa CCM Kirumba.
Klabu ya Simba imeuchagua uwanja wa CCM Kirumba kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Azam FC kutokana na taratibu za usafiri maana awali ingewalazimu baada ya michezo miwili dhidi ya Mashujaa FC na Tabora United warejee Dar Es Salaam halafu warudi tena Mwanza mchezo dhidi ya Geita Gold FC, Februari 12.
Simba imesafirisha bus lake kwa ajili ya safari za kanda hiyo, Simba itasafiri kwa Bus kutoka Kigoma kwenda Tabora na kutoka Tabora kwenda Mwanza, maeneo ambayo hayana usafiri wa ndege.
Simba inashuka dimbani hii leo kuikabili klabu ya mashujaa katika mchezo wa Ligi kuu kandanda Tanzania Bara katika uwanja wa CCM Lake Tanganyika mkoani Kigoma majira ya saa kumi [16:00] Jioni.