Golikipa na Nahodha wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini, Ronwen Williams, ameibuka shujaa wa Taifa lake baada ya kuokoa Penati 4 kati ya 5 dhidi ya Cape Verde kwenye mchezo wa Robo Fainali, AFCON 2023 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Charles Konan Banny.
Ronwen Williams, 32, Anafikia Rekodi ya Golikipa wa zamani wa Timu hiyo ya Taifa na Kocha wa magolikipa wa timu ya Supersport United, Andre Arendse ya Msimu wa mwaka 1996 Wakati Afrika Kusini wanatwaa Ubingwa, Akifikisha Cleansheets 4 kwenye Fainali za AFCON kwa timu ya Afrika Kusini.
Kabla ya mchezo, Andre alisema kuwa
Nafurahia sana ninachokiona kwa Ronwen, Afrika Kusini imepata golikipa haswa baada ya muda mrefu na hii ni kutokana na uzoefu wake pamoja na dhamira yake akitamini kulifikisha Taifa letu mbali kama nahodha. Sijali kama atafikia rekodi yangu.
Williams alidaka penati za Bebe, Willy Semedo, Loras Duarte, Patrick Andrade huku akifungwa na Bryan Texeira pekee lakini upande wa Cape Verde Golikipa Vozinho alidaka penati za Zakhele Lepasa na Aubrey Modiba huku penati za Teboho Mokoena, Mothobi Mvala zikienda kimiani.
Afrika Kusini wanatinga hatua ya Nusu fainali tangu waingie hatua hii mara ya mwisho mwaka 2000, miaka 28 tangu watwae ubingwa wao mwaka 1996. Wanaenda kukutana na Nigeria kwenye hatua hii Tarehe 7.